Habari za Kitaifa

PSC yataka Sh3 bilioni kujaza nafasi za wakongwe wanaostaafu

Na COLLINS OMULO January 26th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

TUME ya Kuwaajiri Watumishi wa Umma (PSC) inataka iongezwe Sh3 bilioni kwenye bajeti kuwaajiri wafanyakazi kujaza nafasi za wakongwe ambao wanastaafu.

PSC inasema kuwa zaidi ya nusu ya walioajiriwa katika utumishi wa umma watastaafu katika muda wa miaka mitano inayokuja.

Asilimia 52 ya watumishi wa umma watatinga umri wa kustaafu kufikia miaka mitano kutoka sasa.

Tume hiyo imekuwa ikikumbatia mageuzi ya kulainisha shughuli zake huku ikilalamika kuwa mgao mdogo pia unaiathiri kwenye utendakazi wake.

Licha ya kwamba inasimamia zaidi ya wizara, idara na mashirika 585, mgao wa bajeti kwa PSC umesalia chini na ule ambao unadhibitiwa.

Mwenyekiti wa PSC anayeondoka Anthony Muchiri alilalamika kwamba mgao mdogo umeathiri uwezo wao wa kuwajibikia majukumu ambayo wameongezewa.

Bajeti ndogo imekuwa ikiathiri ajira kwa wafanyakazi, utekelezaji wa mipango muhimu hasa Nairobi na kaunti nyingine pamoja na ugumu wa kutatua changamoto za watumishi wa umma.

Balozi Muchiri alisema PSC inahitaji bajeti ya kuwaajiri wafanyakazi ili kuzima au kupunguza mwanya wa asilimia 45 ambao umekuwepo kwa muda wa miaka miwili ya kifedha iliyopita.

Pengo

Katika mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2025, PSC ilikuwa na pengo la wafanyakazi 217 kwa sababu ilikuwa ikifanya kazi na waajiriwa 274 ambao ni asilimia 56 ya wafanyakazi wake.

Mwaka huu wa kifedha wa 2025/26, mwanya wa wafanyakazi ni 138, hali ambayo kuna uwezekano finyu kuwa itabadilika miaka inayokuja.

“Wafanyakazi wachache na wafanyakazi ambao wanakaribia kustaafu, ni kati ya changamoto zinazolemaza utendakazi wa PSC,” akasema Bw Muchiri.

“Asilimia 52 ya wafanyakazi watastaafu miaka mitano inayokuja ihali PSC sasa inasimamia ajira katika vyuo vikuu vya umma na Vyuo vya Mafunzo ya Kiufundi,” akaongeza Bw Muchiri.

Kwenye mwaka wa kifedha Juni 30, 2024, Bw Muchiri alisema tume ilikuwa na upungufu wa Sh1.94 bilioni, ambayo ni asilimia 35 ya gharama yake.

Ripoti hiyo inasema PSC ilipokea Sh3.62 bilioni mwaka huu wa kifedha unaokamilika Juni 30, 2026 ila inahitaji Sh3.14 bilioni zaidi ili kufadhili shughuli zake.