Baadhi ya vikwazo vinavyowazuia GenZ kujihusisha na siasa
HUKU uchaguzi mkuu ukikaribia, utafiti mpya umeibua wasiwasi kuhusu idadi ndogo ya vijana wa Gen Z hasa wa kike wanaoingia kwenye siasa.
Hii ni licha ya vijana kuwa kundi kubwa zaidi la wapigakura nchini.
Utafiti huo, uliochambua chaguzi za 2017 na 2022, unaonyesha kuwa chini ya asilimia moja ya viongozi waliochaguliwa katika ngazi ya kitaifa na kaunti ni wanawake wenye umri wa chini ya miaka 35.
Katika uchaguzi wa 2022 kwa mfano, ni wanawake chipukizi 20 pekee waliofanikiwa kuchaguliwa katika nyadhifa mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, changamoto zinazowakumba wanawake hao hazihusiani tu na uwezo wao wa kibinafsi, bali pia mifumo ya kisiasa iliyopo.
Hii ni pamoja na ukosefu wa fedha za kampeni, vizingiti vya vyama vya kisiasa, ushawishi wa wafadhili wasio rasmi, vurugu wakati wa kampeni, kushambuliwa mtandaoni pamoja na kukosekana kwa mifumo ya ulinzi na msaada baada ya uchaguzi.
Akizungumza wakati wa hafla iliyowaleta pamoja wanawake kutoka maeneo mbalimbali, balozi wa EU nchini, Henriette Geiger alisema kuwa baadhi ya wanawake wanapitia dhuluma mbalimbali na hata kutishiwa wakijaribu kuingia kwenye siasa.
“Kuna haja mageuzi yafanywe ili wanawake hasa vijana wa Gen Z wasiwe na hofu wanapoingia kwenye siasa,” alisema Bi Geiger.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kiwango cha mafanikio ya wanawake chipukizi waliogombea kilishuka kutoka asilimia 9 mwaka 2017 hadi asilimia 5 mwaka 2022, licha ya kuongezeka kwa mafunzo yanayolenga uongozi na ufadhili kutoka kwa mashirika mbalimbali ya kiraia.
Watafiti wanasema hali hii inazua maswali mazito kuhusu ufanisi wa mikakati ya sasa ya kuwainua wanawake kisiasa, huku wakisisitiza haja ya mageuzi ya kina katika vyama vya siasa na mifumo ya uchaguzi.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema bila mageuzi ya kimfumo, pengo kati ya ushiriki wa wanawake na uwakilishi wao katika uongozi litaendelea kupanuka, hali inayotishia misingi ya demokrasia shirikishi nchini.