Njaanuari: Watu 2.1m kukumbwa na njaa bei ya bidhaa ikipanda
BEI ya bidhaa muhimu kama unga wa mahindi, sukuma wiki na kabeji inaendelea kupanda kwa kiwango kikubwa kutokana na ukame unaoendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi.
Serikali inakadiria kuwa angalau Wakenya milioni 2.1 wako hatarini kukumbwa na njaa kali na uhaba wa maji iwapo ukame utaendelea.
Takwimu mpya kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) zinaonyesha kuwa athari za mvua hafifu msimu wa vuli tayari zimeanza kuonekana sokoni, hali inayoongeza presha kwa mfumuko wa bei nchini.
Mfumuko huo ulipungua kwa kiasi kidogo hadi asilimia 4.4 Januari 2026 kutoka asilimia 4.5 mwezi uliotangulia.
Hata hivyo, KNBS inasema kuwa kupungua zaidi kulizuiwa na ongezeko kubwa la bei ya kabeji, unga wa mahindi ulioboreshwa, sukuma wiki na viazi, ambazo zilipanda kwa asilimia 9.3, 6.7, 4 na 3.4 mtawalia.
“Katika kipindi cha miezi 12 hadi Januari 2026, bei ya vyakula na vinywaji visivyo na kileo ilipanda kwa asilimia 7.3,” ilisema KNBS.
Kati ya Desemba 2025 na Januari 2026, bei ya wastani ya sukari ilishuka kutoka Sh179.60 hadi Sh174.17 kwa kilo, huku bei ya mafuta ya kupikia ikipungua kwa kiasi kidogo kutoka Sh342.98 hadi Sh342.50 kwa lita.
Bei ya mahindi yasiyopakiwa iliongezeka kutoka Sh69.39 hadi Sh71.28 kwa kilo, sukuma wiki kutoka Sh98.51 hadi Sh102.45 kwa kilo, pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi ulioboreshwa kutoka Sh162.56 hadi Sh173.51, nayo kabeji kutoka Sh65.39 hadi Sh71.47 .
Ongezeko hili la bei ya chakula linajiri baada ya msimu wa mvua za Oktoba hadi Desemba kuwa miongoni mwa misimu mikavu zaidi katika miongo kadhaa, hali iliyovuruga uzalishaji wa mazao na kupunguza upatikanaji wa bidhaa sokoni, hasa mboga na vyakula vinavyotokana na mahindi.
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini (KMD) ilikuwa imetabiri kuwa maeneo mengi ya kaskazini mashariki, nyanda za chini za kusini mashariki na ukanda wa pwani yangepokea mvua chini ya wastani. Hali hiyo ilijitokeza, huku serikali na mashirika ya kibinadamu yakionya kuwa mvua hafifu imevuruga uzalishaji wa mazao, kupunguza malisho na kuathiri mifumo ya usambazaji wa chakula.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame (NDMA), kaunti kadhaa zimeingia katika awamu za tahadhari au hatari ya ukame, huku dalili za awali za uhaba wa chakula zikianza kuonekana hata katika maeneo yaliyokuwa yakichukuliwa kuwa salama awali.