• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Shinikizo Amina ajiuzulu kuhusu mikopo ya HELB

Shinikizo Amina ajiuzulu kuhusu mikopo ya HELB

Na SHABAN MAKOKHA

UTATA unaendelea kushuhudiwa kuhusiana na ulipaji wa zaidi ya Sh7.2 bilioni zilizokopeshwa wanafunzi wa vyuo vikuu na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Vyuo (HELB).

Baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Magharibi wamemtaka Waziri wa Elimu, Amina Mohamed ajiuzulu kutokana na kauli yake kwamba atatumia polisi kuwatafuta wote walioepuka kulipa mikopo.

Kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi na wabunge Beatrice Adagala (Vihiga), Alfred Agoi (Sabatia), Ayub Savula (Lugari) na Didmus Barasa (Kimilili), walimtaka Bi Mohamed kuondoa pendekezo la kuwatumia polisi kupata mikopo hiyo.

Akiongea wakati wa mazishi ya Bw Henry Malova, msaidizi wa Bw Mudavadi katika kijiji cha Mbajo Lugari mnamo Jumamosi, viongozi hao waliitaka serikali badala yake kutafuta pesa zilizoibwa serikalini na kuzitumia kufuta madeni hayo.

“Wanafunzi wengi hawajapata kazi tangu walipoondoka vyuo vikuu. Tunatarajia wapate wapi pesa za kulipa mikopo yao,” aliuliza Bw Mudavadi.

Bi Adagala alisema serikali inafaa kuunda nafasi za kazi kwa vijana ili wanaohitimu wawe na uwezo wa kulipia mikopo yao.

Aliahidi kuongoza maandamano ya kushinikiza kuondolewa kwa Bi Mohamed ikiwa Wizara ya Elimu itatekeleza tishio lake la kuwakamata wanafunzi ambao hawajalipa mikopo ya HELB.

You can share this post!

Caroline Mwatha aliuawa na polisi – Orengo

ODM yataka hoteli ya Ruto ibomolewe

adminleo