NGILA: Teknolojia isiyoenea itazidi kulemaza uzalishaji mali
Na FAUSTINE NGILA
ITHIBATI ya maendeleo ya kiteknolojia nchini Kenya tayari ipo.
Binafsi, nimeshuhudia teknolojia ya juu katika miundo ya simu na kompyuta, mifumo ya malipo ya kidijitali, mawasiliano na matumizi ya roboti yakizidi kurahisisha kazi katika sekta nyingi humu nchini.
Kila mwanauchumi atakubaliana nami kuwa teknolojia ni nguzo muhimu katika kuongeza kiwango cha uzalishaji.
Lakini mbona uzalishaji umepungua katika miongo michache iliyopita, katika kipindi ambapo teknolojia nyingi zilivumbuliwa? Sababu ni nini?
Nikichunguza data katika mataifa mengi, hasa ya Kiafrika, uzalishaji umepungua tangu mwanzo wa karne ya 21. Kumekuwa na sababu nyingi zilizochochea kushuka kwa utengenezaji wa bidhaa viwandani.
Sababu si teknolojia zenyewe bali ukosefu wa kueneza teknolojia hizo kufikia kila mwananchi. Kwa mfano, programu ya “My Dawa” ni nzuri lakini ni Wakenya wangapi wana uwezo wa kumiliki simu ya kisasa ili kufaidika na huduma zake?
Ili kila Mkenya aweze kumudu bei ya simu ya kisasa, basi uchumi wafaa kuimarika kiasi cha kuwa na hela za ziada za kununua vifaa vya kiteknolojia.
Kila Mkenya anatambua kuwa ufisadi umelemaza kila sekta ya uchumi wetu. Lakini hiki si kikwazo pekee cha teknolojia kukosa kuwafikia wananchi wa matabaka ya chini.
Hali hii pia imesababisha kampuni saba zilizokuwa zimeorodheshwa katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE) kuondolewa kutokama na mapato ya chini, licha ya kutumia teknoloia kuimarisha uzalishaji.
Kudorora kwa uzalishaji kunahusiana moja kwa moja na kupanuka kwa pengo la mapato baina ya matabaka mbalimbali ya kiuchumi. Kwa mfano, kampuni ya Safaricom inapata faida kubwa zaidi kwa sababu teknolojia yake ya M-Pesa imeenea kote, huku kampuni pinzani zikiumia.
Hivyo, serikali kupitia kwa Mamlaka ya Ushindani (CAK) yafaa kuondoa vikwazo vinavyozuia ushindani, na kuweka kanuni zinazozima ukiritimba.
Tukiachia kampuni chache umiliki wa soko husika, tutakuwa tunajizuia kufurahia matunda ya teknolojia. Hakuna haja ya wagonjwa kukwama mashinani eti kwa sababu hawana simu za kupata huduma za kiafya kidijitali.
Teknolojia haitakuwa na maana iwapo mamilioni ya wakulima hawana uwezo wa kumiliki simu yenye apu inayowaunganisha na soko la mazao yao, pamoja na kuwaelekeza kwa maduka yenye dawa na mbegu za bei nafuu. Tutazidi kuumia iwapo tutaachia Safaricom idhibiti soko la kutuma hela kidijitali.
Teknolojia inafaa kuwa na ushindani mkali ili kulinda watumizi, lakini hili haliwezekani iwapo teknolojia za kampuni pinzani hazijaenea vizuri.
Sera kuhusu teknolojia nchini zafaa kuboreshwa ili kuvumisha ubunifu na kuueneza hadi mashinani. Kuna raha gani kuwa teknolojia nyingi zisizosaidia kukua kwa uchumi wetu? Teknolojia isiyoenea itazidi kulemaza uzalishaji tusipochukua hatua.