HabariSiasa

FUJO JIJINI: Tutaandamana kupinga vyuo kuongeza karo – Babu Owino

February 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

HUENDA fujo zikashuhudiwa katikati wa jiji la Nairobi na nje ya majengo ya Mahakama ya Milimani Mbunge wa Embakasi Mashariki atakapowaongoza wabunge wenzake na wanafunzi wa vyuo vikuu kuwasilisha kesi ya kuzima nyongeza ya karo vyuoni humo Alhamisi.

Bw Owino Jumatano aliwaongoza wabunge wenzake sita kupinga pendekezo hilo lililotolewa na manaibu chansela wa vyuo vikuu vya umma

“Si haki kwa serikali, kupitia manaibu chansela, kuendesha vyuo vikuu kama vioski. Hatua hii ni kinyume cha kipengee cha 43 cha Katiba kinachosema kila mwanafunzi ana haki ya kupata elimu,” akasema.

“Hii ndio maana Alhamisi saa nne asubuhi kamili mimi, wenzangu hapa na wanafunzi wa vyuo vikuu, tutafika Mahakama Kuu eneo la Milimani kusaka agizo la kupinga utekelezaji wa pendekezo hili la kuongeza karo,” akasema Bw Owino ambaye amewahi kuhudumu kama Mwenyekiti wa Chama cha Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi kwa mihula mitatu.

Aliandamana na wabunge; Brighton Yegon (Konoin, Jubilee), Mohammed Ali (Nyali, asiyedhaminiwa na chama), Samuel Atandi (Alego Usonga, ODM), Charles Nguna (Mwingi Magharibi, Wiper), Antony Oluoch (Mathare, ODM) na John Paul Mwirigi (Igembe Kusini, asiyedhaminiwa na chama).

Manaibu Chansela hao wakiongozwa na mwenzao anayesimamia Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya (TUK) walipendekeza kuwa karo hiyo iongezwe kutoka Sh16,000 hadi Sh48,000 kwa kila mwanafunzi kila muhula.

Bw Yegon aliitaka serikali kufutilia mbali karo zinazotozwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kuhakikisha kuwa imeziba mianya ya wizi wa pesa za umma kupitia ufisadi.

“Ikiwa serikali kuu itazua kero la ufisadi katika sekta ya umma ninaamini kuwa itaeza kufadhili elimu katika vyuo vikuu vya umma bila kutoza karo. Elimu ndio kichochea cha maendeleo na haifai kuwa ghali, haswa kwa Wakenya masikini,” akasema.

HELB

Wabunge hao pia walipinga wazo la Bodi ya Kutoa Mikopo kwa Elimu ya Juu (HELB) la kutumia polisi kuwasaka Wakenya waliokwepa kulipa mkopo huo.

“Serikali inafaa kuhakikisha kuwa wahitimu wa vyuo vikuu wanapewa kazi kwanza kabla ya kuhitajika kuanza kulipa mkopo huo.” akasema Bw Atandi.

Bw Owino aliahidi kuwasilisha mswada bungeni kuilazimisha HELB kuondoa riba ya asilimia nne ambayo waliofaidi na mkopo huo.

“HELB inafaa kuondoa hii riba kwa sababu bodi hii sio benki ya kibiashara. Pia napendekeza katika mswada wangu kwamba kiwango cha mkopo uongezwe kutoka Sh40,000 hadi 100,000 kila mwaka,” akasema.

Wanafunzi wa vyuo vikuu wameahidi kufanya maandamano mnamo Machi 4 kupinga mpango huo wa kuongezwa kwa karo, wakisema utawaathiri wengi wao ambao wanatoka jamii masikini.