Wafisadi kwenye kaunti waingiwa na kiwewe EACC ikibisha
Na KENNEDY KIMANTHI
HOFU imeibuka katika serikali za kaunti kufuatia hatua ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuanzisha msako mkali dhidi ya magavana na wafanyakazi wa kaunti wanaoshukiwa kujihusisha kwa ufisadi.
EACC imesema hivi karibuni upelelezi wao utakamilika baada ya kukagua ripoti za Mhasibu Mkuu ambazo zimetaja maafisa wakuu na wa ngazi za chini wa kaunti kushiriki ufisadi na ufujaji wa pesa za umma.
Karibu kila serikali ya kaunti imesemekana kukiuka sheria za utoaji zabuni, miongozo ya kuajiri wafanyakazi kwa kuwapa wandani na jamaa kazi, kupoteza fedha zinazokusanywa kutoka kwa ushuru katika kaunti au kulipa wafanyakazi hewa.
Hali hii imepelekea asasi husika za kupambana na ufisadi kulenga darubini zao katika serikali hizo ili kuadhibu wanaohusika kwa wizi na uharibifu wa mabilioni ya pesa.
Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Twalib Mbarak alisema Jumanne kwamba Mhasibu Mkuuu ameonyesha kuna hali mbaya ya uwajibikaji na uwazi katika serikali za kaunti kuhusu usimamizi wa fedha.
Ripoti zilizopo zinaonyesha makosa makubwa katika utumizi wa pesa za umma katika kaunti na hivyo basi kuwepo uwezekano wa wizi na utumizi mbaya wa fedha za mlipa ushuru.
Inasemekana madiwani na maafisa wa afisi za magavana hushirikiana kujinufaisha kutokana na fedha wanazopaswa kusimamia.
“Ufujaji mkubwa uko katika kaunti. Njia mojawapo ya kuondoa ufisadi katika kaunti ni kwa EACC kuanzisha misako ya ghafla. Macho yetu sasa yanalenga kaunti na tunajua maafisa fisadi wanajiepusha na mabenki kwa sababu ya sheria kali zilizopo kuhusu kuweka na kutoa fedha katika benki na badala yake wanazificha manyumbani mwao,” akasema kwenye mahojiano katika Runinga ya Citizen usiku wa kuamkia jana.
Kulingana na Bw Mbarak, kuna uwezekano maafisa wa EACC watamfikisha gavana mmoja katika makao yao makuu Nairobi kuandika taarifa, ingawa hakufichua ni gavana yupi wala maafisa wanaochunguzwa.
Wiki iliyopita, wapelelezi wa EACC walivamia na kufanya msako katika nyumba za Gavana wa Samburu Moses Kasaine zilizo Samburu na Nairobi wakitafuta stakabadhi zinazohusiana na utumizi wa Sh2 bilioni.
Mwaka uliopita, aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero alifikishwa mahakamani kushtakiwa kwa utumizi mbaya wa mamlaka na kuhalalisha pesa haramu.
Duru katika tume ya ufisadi zilizema kuna magavana wengine wawili walio mamlakani wanalengwa kwa madai ya kuhusika katika ufujaji wa mamilioni ya pesa hasa wakati wa kununua mali ya umma, na utumizi mbaya wa mamlaka wanazoshikilia.
Bw Mbarak alisema tume hiyo inaamini kuna ushahidi wa kutosha dhidi ya magavana hao kwani upelelezi ulifanywa kwa kina.
“Zaidi ya hayo, tulielewana na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kwamba wapelelezi wetu wawe wanashirikiana na mawakili wa afisi yake ili tuwe na kesi thabiti,” akasema.
Ripoti za Mhasibu Mkuu kila mwaka huonyesha jinsi mabilioni ya pesa za umma zinapotea katika kaunti.