Siendi popote, Jumwa aambia ODM
CHARLES LWANGA na FADHILI FREDRICK
Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa amepuuzilia mbali kufurushwa katika chama cha ODM huku mbunge wa Msambweni Suleiman Dori akishukuru chama hicho kwa kumpa nafasi ya kujitetea.
Bi Jumwa aliwaambia wakazi wa eneobunge lake kwamba hakuna uchaguzi mdogo utakaofanyika baadhi ya watu wanavyodai.
“Sihitaji kuomba mtu yeyote msamaha kutokana na uamuzi wangu, kura ni za Malindi na sisi ndio Wanamalindi na ningependa kuwaambia kuwa hakutakuwa na uchaguzi wowote hapa, wafanyabiashara waendelee na shughuli zao bila woga,” alisema.
Bw Hossea Chome, ambaye ni naibu mwenyekiti wa chama cha ODM eneobunge hilo na shabiki mkuu wa Bi Jumwa pia alipuuzilia mbali uamuzi wa chama kufurusha Bi Jumwa.
“Chama kimekiuka haki cha mama wetu na wakazi wa Malindi ambao tulimchagua na tutasimama naye hadi mwisho,” alisema na kumwambia Bi Jumwa asibabaike kwa sababu wakazi wako nyuma yake.
Haya yanajiri siku moja baada ya baraza la uongozi wa chama cha ODM kupitisha uamuzi wa kamati ya nidhamu kumfurusha Bi Jumwa kwa kukosa nidhamu.
Bi Jumwa alisema kuwa mvua inyeshe au kiangazi kijiri, atabaki kuwa mbunge wa Malindi akiongeza kuwa atakabiliana na chama cha ODM kwa kumfurusha.
“Mungu akishasema, wanenaji wengine wote wanakuwa wapikaji kelele, wale Nairobi ni wapigaji kelele,” alisema na kuongeza: “Nitaendelea kutumikia wakazi na kuleta maendeleo yatakayoinua uchumi ya wakazi.”
Bi Jumwa alisema hangekapinga kufurusha kwake kama ODM kingefuata sheria.
“Mimi si mtu wa kutishwatishwa, nimewaheshimu na nitaendelea kuwaheshimu hasa kinara wa chama, nataka niwaambie kuwa mimi si mtu wa kutishwa tishwa,” alisema.
Bi Jumwa alisema sasa amekuwa imara maradufu kutokana na unyanyasaji huo akiongeza kuwa “hatakubali kuhangaishwa na mtu yeyote kubadilisha msimamo wake kisiasa.”
“Wale wanaopanga matanga yangu ninataka kuwaambia kuwa mimi ndio nitakayekula katika matanga yao,” alisema na kuongeza “Aisha Jumwa hatabadilika na atabaki kuwa yuleyule leo na kesho.”
Wakati huohuo, Bi Jumwa ambaye alikuwa ameandamana na mamia ya wakazi alimwambia Kinara wa ODM Raila Odinga aeneze amani na upatanisho mjini Malindi badala ya kuleta fujo za kisiasa.
Akizungumza na wananchi katika Shule ya Wasichana ya Dori huko Gazi Jumamosi, Bw Dori alisema alifurahishwa na uamuzi wa chama hicho kwa kumpa fursa ya kufika mbele ya kuu la chama hicho baada ya siku 60.
Hususani Bw Dori alitoa shukrani za dhati kwa Bw Odinga kwa hekima yake katika kutatua migogoro katika chama hicho.
Pia Bw Dori alisisitiza kwamba yeye bado ni mwanachama wa ODM na kwamba yuko tayari kufanya kazi na viongozi wengine kutumikia watu wa Msambweni.
“Nataka niwajulishe Wakenya kwamba mimi bado ni mwanachama wa ODM na nitaendelea kutekeleza kazi yangu katika kuwahudumia watu wa Msambweni kama mbunge wao katika chama cha ODM,” akasema.
Alisema uamuzi uliofikiwa na baraza kuu la chama na kumpa fursa ya kuongoza sio kwa nguvu zake ila ni kupitia uwezo wa Mungu katika kumnasua katika matatizo yaliomkabili.
“Ninataka kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kuwa mwaminifu kwangu na kunisaidia kutatua mgogoro wa chama kwa amani na kunipa nguvu za kuendelea kuhudumia wananchi wa Msambweni,” akasema.