17/06/2019

OBARA: Serikali iingilie kati mikopo hii ya kidijitali

Na VALENTINE OBARA

KWA miaka kadhaa sasa, Kenya imeshuhudia maendeleo makubwa katika utoaji wa huduma za kifedha.

Ustawishaji wa huduma zinazotolewa na mashirika ya kifedha umetokana na ukuaji wa teknolojia za kisasa hasa Teknolojia za Habari na Mawasiliano (ICT).

Nakumbuka vyema wakati huduma za fedha kwa njia ya simu zilipoanzishwa nchini humu kwa mara ya kwanza ulimwenguni katika mwaka wa 2007, baadhi ya mabenki hayakupendezwa na mpango huo kwa kuwa ilidhaniwa ungewaharibia biashara.

Miaka 12 baadaye, benki zimo kwenye mstari wa mbele kubuni mbinu za kila aina ili kujifaidisha kutokana na teknolojia hii.

Kinachoshuhudiwa ni kwamba utoaji wa huduma za fedha umerahisishwa mno na benki zinaweza kufikia idadi kubwa zaidi ya wateja kwa urahisi.

Miongoni mwa huduma kuu ambazo zimeshamiri kwa sababu ya teknolojia hii ni utoaji wa mikopo.

Imekuwa rahisi sana kwa Wakenya wa matabaka ya chini kupata mikopo ikilinganishwa na jinsi ilivyokuwa katika miaka ya jadi.

Hivi sasa kuna mikopo ambayo kile mwananchi anahitaji kuwa nacho ni laini ya simu iliyosajiliwa inavyotakikana kisheria.

Manufaa haya hayajakuja bila changamoto yake, kwani matokeo ni kuwa Wakenya wameishia kuchukua mikopo tele inayotumiwa kiholela.

Kwa kawaida mkopo unaochukuliwa kwa njia bora huhitaji mteja kueleza kile ambacho anaenda kufanyia fedha hizo na ikiwezekana aonyeshe thibitisho la nia yake.

Lakini hivi sivyo katika huduma za fedha kwa njia ya simu.

Ingawa kuna Bodi ya Kusimamia Mikopo (CRB) ambayo huamua kama mtu anastahili kupokea mikopo kwa msingi wa kama alilipia mikopo mingine aliyochukua awali, hii haitoshi kudhibiti utumizi bora wa fedha kwa wananchi.

Kumekuwa na visa ambapo wateja wamefikia kiwango cha kukwama kabisa kifedha kwa sababu walichukua mikopo mingi wakashindwa kulipia na wanapohitaji kukopa fedha kwa dharura, hawana uwezo huo kwa sababu CRB imewaorodhesha kama wakwepaji wa kulipa madeni.

Itakuwa vyema kama asasi husika za serikali zitashirikiana kutafuta sera au hata sheria za kusimamia mifumo hii mipya ya utoaji mikopo.

Hii inahitajika ili fedha hizi ziwe zinachukuliwa tu kwa kuzingatia mahitaji ya mteja, wala isiwe mikopo inapeanwa tu kiholela kwa yeyote atakaye.

Tunafahamu mabenki huwa na lengo la kupata faida na hakika, faida zao huzidi kuongezeka kadri na jinsi mteja anavyochelewa kulipa madeni yake kwa sababu riba itaongezeka.

Lakini hakuna utu kwa binadamu yeyote yule kutumia ujinga au upumbavu wa mwingine kujitajirisha.

Hatua sawa na hii inapaswa pia kuchukuliwa kudhibiti programu za simu ambazo zimeundwa kwa minajili ya utoaji mikopo kwa umma.

Programu hizo ambazo nyingine hazijulikani hata zilikotoka wala zinavyosimamiwa, zinazidi kusababisha mzigo mkubwa wa madeni kwa wananchi wasio na nidhamu katika matumizi ya fedha.