Habari MsetoSiasa

Afueni kwa Jumwa

March 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MBUNGE wa Malindi Bi Aisha Jumwa anayepigwa na mawimbi makali ya kisiasa alipata afueni Jumanne baada ya hatua ya kumfukuza katika chama cha Orange Democratic Movement (OMD) kubatilishwa.

Jopo la Kuamua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PDDT) lilitia breki hatua ya ODM kumtimua Bi Jumwa chamani hadi kesi aliyowasilisha isikizwe na kuamuliwa.

Na wakati huo huo mwenyekiti wa PDDT Bw Kyalo Mbobu alizima kwa muda hatua ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Bi Anne Nderitu kufuta jina la Bi Jumwa katika Sajili ya chama cha ODM.

Kufutwa kwa jina lake kuna maana kwamba atakipoteza kiti chake cha ubunge mara moja.

Wadadisi wanasema chama cha ODM kilimtimua chamani Bi Jumwa kwa kuunga mkono azma ya naibu wa Rais William Ruto kuwania urais 2022 kwa tikiti ya chama cha Jubilee.

ODM kikimtimua chamni kilitumia kipengee nambari 14 cha katiba kinachokataza mmoja kuunga mkono chama kingine cha kisiasa ambacho hakikudhamini uteuzi wake.

ODM kilisema Bi Jumwa anaunga mkono Bw Ruto ilhali angali mwanachama na mbunge aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM.

Bw Mbobu aliratibisha kesi hiyo ya Bi Jumwa kuwa ya dharura na kuamuru isikizwe Machi 8.

Bw Mbobu alimwagiza Bi Jumwa awakabidhi washtakiwa nakala za kesi aliyowasilisha ndipo wajibu madai dhidi yao.

Katika kesi hiyo Bi Jumwa amekishtaki chama cha ODM na Msajili wa vyama vya kisiasa Bi Anne Nderitu.

Bi Jumwa alimweleza Bw Mbobu kwamba chama cha ODM kilikandamiza haki zake kwa kutompa fursa ya kujitetea.