UVUMBUZI: Uchapishaji wa 3D unavyotumika kuunda upya viungo vya mwili
Na PAULINE ONGAJI
AMEVUMBUA teknolojia ambayo inasaidia madaktari wa upasuaji kutekeleza kazi zao sio tu kwa urahisi, bali pia kwa usahihi na hivyo kuwezesha wagonjwa kupona upesi.
Ni jitihada zake Bw Christopher Muraguri, ambaye kupitia Micrive Infinite, kampuni aliyoanzisha kwa ushirikiano na Bw Mandela Kibiriti amevumbua teknolojia ya kuumba mifano ya sehemu za mwili inayosaidia madaktari kujiandaa kabla ya upasuaji na kutumia vipimo kamili.
Hasa mchango wa Bw Muraguri unahusisha ufinyanzi wa viungo vya mwili na hasa kichwa kwa kutumia aina spesheli ya plastiki, mifano ambayo inafanana kabisa na viungo kamili vya mgonjwa mhusika, kimaumbile na hata kwa vipimo.
Kwa kawaida Bw Muraguri huafikia haya kwa kutumia data kutokana na picha za CT scan, kisha anatumia taarifa hizi kuunda mfano wa sehemu husika kwa kutumia aina maalum ya plastiki ya Z-PETG, sehemu bandia za mifupa au vipande vya chuma kisha umbo hili linafanywa kuwa ngumu na kuwekwa meno na hivyo kufanana kabisa na sehemu ya mwili. “Viungo hivi vyaweza undwa kuambatana na vipimo kamili vya mgonjwa husika,” anaongeza.
Shughuli hii hufanyika kwa awamu ambapo mgonjwa anamtembelea daktari ambaye anatambua maradhi, kisha Bw Muraguri (Micrive) anahusishwa ili kuchukua kipimo cha mwili na kiungo husika, kwa mwongozo wa mpasuaji.
Baadaye, kwa kutumia printa maalum ya kimatibabu ya grade 3D, mfano wa umbo la sehemu iliyoathirika unatumika kuunda umbo kamili kwa kutumia plastiki.
Bali na kusaidia kuandaa madaktari kabla ya upasuaji, teknolojia hii inachangia pakubwa katika shughuli za kuumba upya sehemu za mwili zilizoondolewa kutokana na maradhi kama vile kansa, majeraha na udhaifu wa kimaumbile
Huku akiwa ameunda zaidi ya maumbo 150 kufikia sasa, wamehusika katika shughulu zote za upasuaji ambazo zimeendelezwa kwa kutumia teknolojia ya uchapishaji wa 3D nchini katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Robert Mbuthia, 43, ni mojawapo ya watu ambao wamenufaika kutokana na teknolojia hii. Tangu utotoni alikuwa akikumbwa na hali inayofahamika kama severe malocclusion, kwa lugha ya kitaalamu, au hitilafu katika mfuatano wa meno, suala liliathiri jinsi meno ya juu na ya chini zinavyokutana, taya zinapojifunga.
Ni hali ambayo mwanzoni aliweza istahimili, lakini muda ulivyokuwa ukisonga, mambo yalizidi kuwa mabaya na kuathiri maisha yake kabisa.
“Nilipozidi kukomaa kiumri nilikumbwa na uchungu mwingi hasa wakati wa kutafuna. Meno ya sehemu ya juu ya upande wa kulia yalikuwa yakidunga ufizi wa chini kila nilipokuwa nikitafuna. Kutokana na hili nilijipata nikitafuna kwa kutumia upande wa kushoto pekee ambapo pia singeweza tafuna vyakula vigumu,” anaeleza.
Kando na hayo, meno yake yalikuwa yakisonga upande wa kushoto na kuacha nafasi kati kati, kiasi cha kwamba kila alipokuwa anatafuna chakula, kulisalia vipande vikubwa vya chakula mle.
Kulingana naye, madaktari walimwambia kuwa mambo yalikuwa mabaya hata zaidi kutokana na sababu kuwa alikuwa katika umri wa makamo, suala ambalo lingetatiza shughuli za kurekebisha hali hiyo.
“Kutokana na sababu kuwa nilikuwa mkomavu, ilikuwa ngumu kurekebisha hali hii, ikilinganishwa na pengine iwapo ningekuwa katika umri wa kubalehe ambapo meno yote hayangekuwa yameota,” anaeleza.
Suluhisho lilikuwa kufanyiwa upasuaji unaojulikana kama orthognathic surgery, shughuli ambayo hurekebisha mpangilio wa meno kwenye utaya, upasuaji ambao ulifanyika Desemba 1, 2017.
Kwa Dkt Muthoni Njuguna, tatizo lake lilikuwa Fibrous dysplasia, hali ambapo nafasi ya mfupa wa kawaida na uboho inachukuliwa na tishu ya unyuzi na kuunda mfupa dhaifu ambao waweza kupanuka.
Ni hali ambayo alikuwa nayo tokea utotoni na kufanya utaya wake kuonekana mkubwa zaidi tofauti na kawaida.
“Hali hii ilifanya nionekane kuwa na kasoro ambapo ilikuwa kawaida kwa watu kunikodolea macho, suala ambalo hasa liliwatia hofu wazazi wangu. Kwa hivyo nililazimika kufanyiwa upasuaji mara kadha katika harakati za kurekebisha tatizo hili,” anasema.
Mapema mwaka jana upasuaji mkuu ulifanywa na japo bado yuko katika harakati za kurejea hali ya kawaida, ulikuwa wa kipekee ambapo anatarajiwa kupata nafuu kati kati mwa mwaka huu.
Kulingana na Profesa Symon Guthua, mtaalam wa upasuaji anayehusika na kutibu maradhi, majeraha na kasoro sehemu za kichwa, shingo, uso, taya na tishu mdomoni, katika Chuo Kikuu cha Nairob, upasuaji katika hali zote mbili ulikuwa mgumu ambapo usahihi ulihitajika.
Anasema kutokana na teknolojia hii, yeye pamoja na wataalam wengine waliohusika waliweza kutambua tatizo, kujua mbinu za kutumia kufanya upasuaji na hata kupanga kabla ya shughuli hiyo kuanza.
Ni suala ambalo asema linaimarisha usalama wa wagonjwa hasa ikizingatiwa kwamba kabla ya kuanza shughuli hii wana ufahamu kuhusiana na sehemu halisi zilizoathirika, kumaanisha kwamba uwezekano wa kufanya makosa ni finyu sana.
“Kwa mfano, upasuaji uliofanyiwa Dkt Muthoni ulikuwa wa kwanza duniani kote, na pasipo maumbo haya basi ingekuwa ngumu kujua nini hasa cha kufanya kwani hatuna mwongozo wa shughuli za upasuaji za awali afikia haya,” anaeleza.
Mbali na hayo, Prof. Guthua anasema kwamba shughuli za kuelimisha wagonjwa zimerahisishwa kwani kabla ya upasuaji kuanza wanaelezwa kuhusu utaratibu utakaohusika, huku wakiwa wameshika umbo sawa na sehemu ya mwili wao iliyoathirika, ikilinganishwa na kuwaeleza kwa kutumia picha.
“Pia hauhitaji kumsumbua mgonjwa kwa ziara za kila mara hospitalini kwani pindi baada ya kupata umbo la sehemu iliyoathirika tunaweza jiandaa kabla ya upasuaji, pasipo mgonjwa kuwepo,” anaongeza.
Kwa upande mwingine, anasema kwamba, pia wagonjwa wanaridhika kabla ya upasuaji kwani wanaweza pata picha kamili ya utaratibu huo hata kabla ya kuanza, suala linalopunguza wasiwasi.
Dkt Margaret Ndung’u-Mwasha, daktari wa meno na mtaalam wa viungo bandia vya mdomoni, na ambaye ametumia teknolojia hii mara kadha, anasema teknolojia hii inawawezesha kuunda viungo bandia vitakavyochukua nafasi ya vile halisi vilivyoathirika, hata kabla ya upasuaji.
“Hii inamaanisha kwamba shughuli yote ya upasuaji na kuweka viungo bandia inafanywa wakati mmoja katika chumba cha upasuaji. Awali, shughuli ya kuunda viungo bandia ilichukua muda kwani ilikuwa lazima tuanze kufanya mipango ya kuvisanifu baada ya upasuaji, kumaanisha kwamba mgonjwa alihitajika kukaa muda mrefu kabla ya kumaliziwa upasuaji, suala lililofanya ichukue muda mrefu kabla ya kurejelea hali yake ya kawaida,” anaeleza.
Bw Muraguri alipata msukumo wa kuvumbua teknolojia hii Novemba mwaka wa 2015, baada ya kuhusika kwenye ajali mbaya ya barabarani iliyoacha mguu wake wa kushoto na majeraha mabaya.
“Picha za skani hazikotoa maelezo kamili kuhusiana na kiwango cha majeraha niliyopata, na hivyo upasuaji ambao ungechukua masaa mawili pekee uliishia kuchukua masaa sita. Pia, nilitakikana kukaa na plasta kwa wiki sita pekee lakini nikadumu nayo kwa miezi miwili. Hii ni kando na kuwa bili ya hospitali ilikuwa imeongezeka,” anaeleza.
Swali lililomjia lilikuwa ni vipi angefanya kuimarisha usahihi na hivyo kupunguza muda wa upasuaji na gharama za matibabu? Na hivyo alianza kufanya utafiti, na majuma kadha baadaye alikuwa ashakamilisha kufinyanga muundo wa mguu wake.
“Nilipomuonyesha daktari wa upasuaji muundo wa mguu wangu alifurahi ambapo alinitambulisha kwa wenzake. Muundo huu uliwarahisishia kazi walipokuwa wakiushughulikia mguu wangu na matokoeo yalikuwa mazuri,” anasema.
Baada ya hapa alijitosa katika utafiti wa ziada uliochukua miaka miwili, mara hii akishirikiana na Prof. Guthua.