Habari Mseto

Mbunge apendekeza vituo zaidi vya kurekebisha tabia, maadili Kiambu

March 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

KILA kaunti ndogo Kiambu inapaswa kuwa na kituo cha kurekebisha tabia na maadili, amesema mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Gathoni Wa Muchomba.

Kulingana na mbunge huyu ni kwamba hatua hii itsaidia kunusuru waathiriwa wa pombe na dawa za kulevya.

Wa Muchomba amesema kuna waathiriwa wengi lakini kituo anachoongoza ambapo ni mlezi; cha Mamacare, kilichoko Wangunyu, kina nafasi ndogo kuwasajili wote kwa wakati mmoja.

“Tuna zaidi ya wagonjwa 2,700 (akimaanisha waathiriwa) wanaosubiri kujiunga na kituo cha Mamacare, lakini kina uwezo wa kusitiri 200 pekee kwa wakati mmoja,” ameambia Taifa Leo.

Ili kufanikisha juhudi za kuokoa waathiriwa, mbunge huyu ameihimiza serikali kufungua kituo katika kila kaunti ndogo Kiambu.

Mwakilishi Mwanamke wa Kiambu, Bi Gathoni Wa Muchomba. Picha/ Maktaba

“Ninasihi serikali ifungue kituo cha kurekebisha tabia na maadili katika kila kaunti ndogo ili tuweze kusaidia vijana wetu,” ameeleza.

Mwaka 2018, chini ya Mamacare, Wa Muchomba alikuwa ameahidi kufungua vituo zaidi eneo la Thika na Ruiru.

Jumatatu Machi 4 kituo hicho kilipokea waathiriwa 200 ambao wapitia mafunzo ya miezi tisa kuwasaidia kuacha unywaji wa pombe na dawa za kulevya.

Desemba 2018 waliokuwa walevi 77 walifuzu baad ya kuonekana wamerebekika, katika hafla iliyohudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta.

‘Githeri Man’

Martin Kamotho Njenga maarufu ‘Githeri Man’, mwanamume aliyepata umaarufu wakati wa uchaguzi mkuu wa 2017 kwa kula githeri akiwa kwenye foleni ya kupiga kura, alikuwa mmoja wa waliohitimu baada ya kulemewa na unywaji wa pombe.

Gavana Ferdinand Waititu amekuwa akiendesha mradi sawa na wa Bi Wa Muchomba, ingawa wake waathiriwa wamekuwa wakifanya kazi ya kufagia barabara, kusafisha mitaro na kufyeka na kulipwa Sh400 kila siku.

Licha ya kukosolewa na baadhi ya viongozi Kiambu wakiutuhumu kutumika kufuja mamilioni ya pesa, Waititu ameutetea vikali akihoji ulisaidia kubadili vijana.

Mpango huo, unaojulikana kama Kaa Sober, ulianzishwa Machi 2018 na ulifadhiliwa na serikali ya kaunti ya Kiambu.

Februari 2019 waengine wapatao 5,200 walifuzu na kupewa kitita cha Sh20,000 kila mmoja, gavana akisema pesa hizo ni mtaji wa kuwasaidia kufungua biashara.

Alisema vijana wengi Kiambu wanajihusisha na unywaji wa pombe kwa sababu ya kukosa kazi.

Aliendelea kueleza kwamba pesa walizopokea ilikuwa mojawapo ya ahadi yake wakati wa kampeni 2017 kutafutia vijana wa Kiambu nafasi za ajira.

Kaunti hiyo ni baadhi ya zilizoathirika pakubwa kwa unywaji wa pombe, hasa ile haramu.