Wauguzi sasa kuajiriwa kwa kandarasi
Na JILL NAMATSI
WAUGUZI sasa watakuwa wakiajiriwa kwa kandarasi kufuatia mwafaka ambao ulifikiwa jana kati ya Serikali Kuu na zile za kaunti.
Hatua hiyo inalenga kukabili migomo ya wauguzi ya mara kwa mara, ambayo imeathiri sana sekta ya afya nchini.
Mwafaka huo uliafikiwa jana kwenye mkutano uliofanyika katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, ambapo ilikubaliwa kwamba kuna hatua za haraka zinazopaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha wagonjwa hawaathiriwi tena na migomo inayotokea.
Kwenye taarifa ya pamoja, Waziri wa Afya Sicily Kariuki na mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya ,walikubaliana kuhusu mikakati ya kuimarisha huduma katika hospitali za umma nchini.
Walikubaliana kwamba, muuguzi yeyote anayeajiriwa katika kiwango cha kaunti na kitaifa ataajiriwa kwa njia ya kandarasi.
“Kulingana na makubaliano yetu, kanuni hii itaanza kutekelezwa mara moja,” wakasema kwenye taarifa.
Hatua hiyo ni pigo kubwa kwa wauguzi, kwani itakuwa vigumu kwao kujiunga na vyama vya kutetea maslahi yao.
Hilo pia linaweka hatari ajira zao, kwani hilo pia linamaanishi sio lazima kupewa upya kandarasi baada ya kuisha.
Ili kutekekeza hilo, Tume ya Kuwaajiri Watumishi wa Umma (PSC) iliagizwa kubuni utaratibu ambao utazingatiwa kwenye ujiri wa wauguzi hao.
Kulingana na wawili hao, Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) vile vile itajumuishwa katika utekelezaji wa utaratibu huo.
Pande hizo mbili pia zilikubaliana kwa pamoja kuwaadhibu wauguzi ambao hawakurejea kazini kufikia Februari 15 kama walivyoagizwa.
Wauguzi walianza mgomo wao mnamo Februari 4 wakishinikiza kuongezwa mishahara na marupurupu yao.