Habari MsetoSiasa

Wabunge kukagua ufaafu wa Magoha kuwa waziri

March 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na DAVID MWERE

BUNGE la Kitaifa lina siku 21 kuidhinisha au kukataa uteuzi wa Prof George Magoha kama Waziri wa Elimu.

Prof Magoha aliteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuchukua mahali pa Amina Mohammed, aliyehamishiwa katika Wizara ya Michezo, iliyokuwa imesimamiwa na Rashid Echesa, ambaye alifutwa kazi wakati wa mageuzi katika Baraza la Mawaziri mnamo Ijumaa.

Prof Magoha alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) kabla ya kuteuliwa kuwa waziri.

Akitangaza uteuzi wa Bw Echesa, Spika wJustin Muturi aliwaambia wabunge kuwa wana hadi Machi 26 kuidhinisha au kukataa uteuzi wake.

Hii inamaanisha kuwa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu, ambayo inasimamiwa na Mbunge wa Tinderet, Julius Melly itamchunguza na kumwidhinisha au kumkataa Prof Magoha, ambaye wakati mmoja alikuwa Makamu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi.

“Kwa kuzingatia hili, kamati inafaa kufanya haraka kumwarifu mteuliwa na umma kuhusiana na mahali na wakati wa shughuli ya kuidhinishwa kwake,” alisema Bw Muturi.

Ikiwa wabunge watamwidhinisha, Spika atawasilisha jina lake kwa Rais kwa uteuzi rasmi.

Prof Magoha, ni maarufu kwa mageuzi bora aliyoleta KNEC, ambayo yalisababisha kupungua kwa visa vya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa.

Katika Wizara ya Elimu, anatarajiwa kuhakikisha kuwa mtalaa mpya umefaulu.

Prof Magoha pia anatarajiwa kuhakikisha kuwa mradi wa dijitali umefaulu na kutatua mzozo kati ya Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) na walimu kuhusu mishahara na masuala mengine ya utendaji kazi.