HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Ziara ya Ruto yafichua ushindani mkali ngomeni

Na BARNABAS BII October 22nd, 2026 Kusoma ni dakika: 3

ZIARA ya siku 10 ya Rais William Ruto katika ngome yake ya kisiasa ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa imefichua ushindani unaozidi kuongezeka ndani ya chama tawala cha UDA huku wanasiasa wakiwania ushawishi wake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Ziara hiyo iliyohusisha uzinduzi wa miradi ya maendeleo na sherehe za Mashujaa Day, ilidhihirisha makundi yanayojipanga kuwania viti vya magavana, wabunge na nyadhifa nyingine za uchaguzi ujao.

Ingawa UDA ina uungwaji mkono mkubwa katika eneo hilo, tofauti za viongozi wanaotaka tiketi ya chama zimeanza kuwa changamoto kwa Rais Ruto, hasa ikizingatiwa kuwa uteuzi wa chama unaweza kuamua hatima ya wengi wao.

Mchambuzi wa siasa wa Eldoret, David Kosgei, alisema wagombea wanajitahidi kupata nafasi ya kuzungumza na Rais wakiamini kuwa baraka zake zitawasaidia kupata kura.

“Wagombea wote wanatafuta kuteka umakini wa Rais Ruto kwa matumaini kuwa mkakati huo utawasaidia kupata kura,” alisema.

Katika kaunti ya Uasin Gishu, ushindani umejikita kati ya makundi yanayohusishwa na Gavana Jonathan Bii Chelilim na Seneta Jackson Mandago.

Kambi ya Mandago inajumuisha Katibu katika Wizara ya Utalii Julius Bitok, ambaye anajaribu kwa mara ya tatu kuwania ugavana, Mbunge wa Soy David Kiplagat na Mbunge wa Kesses Isaac Rutto.

Kwa upande mwingine, kundi la Gavana Bii inahusishwa na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi na washirika wake wa kisiasa.

Hata hivyo, ushindani huo hauhusu uchaguzi wa 2027 pekee, bali pia nani atakuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa jamii ya Wakalenjin baada ya Ruto kuondoka kwenye ulingo wa siasa.

Mchambuzi Benjamin Kirwa alisema makundi hayo yanaashiria mapambano makubwa yanayoweza kulipuka iwapo viongozi watashindwa kudhibiti tofauti zao.

“Mapambano ya kisiasa hayahusu uchaguzi mkuu wa 2027 pekee, bali pia nani atakuwa msemaji wa Wakalenjin baada ya Rais Ruto kuondoka kwenye ulingo wa siasa,” alisema.

Mvutano ulionekana wazi zaidi katika kaunti ya West Pokot, ambapo makundi mawili yanapigania ushawishi kuelekea uchaguzi wa ugavana.

Kundi la 5G linahusishwa na aliyekuwa gavana John Lonyangapuo, huku kundi la Message likihusishwa na Mbunge wa Sigor David Pkosing.

Makundi hayo yanapigania ushawishi ndani ya UDA licha ya viongozi wao kuhusishwa na Kenya Union Party (KUP), ambacho kimehamia upande wa UDA.

Kundi la 5G linajumuisha Seneta Murgor, Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong, Mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto, Mwakilishi wa Wanawake Rael Kasiwai, aliyekuwa Mbunge wa Kacheliba Mark Lomunokol na aliyekuwa Katibu wa wizara James Teko.

Mrengo wa Messag nao unajumuisha Gavana Simon Kachapin, Mbunge wa Kacheliba Titus Lotee, aliyekuwa Mbunge wa Sigor Philip Rotino, Balozi wa Kenya nchini Zambia Lillian Tomiton, Naibu Gavana Robert Komolle, MCA wa Sekerr Jane Mengich, Naomi Kendagor na Spika wa Bunge la Kaunti Fredrick Kaptui, pamoja na madiwani wengine.

Mchambuzi wa siasa Joshua Kosgei alisema kupata tiketi ya UDA na kuungwa mkono na Rais kunaweza kuwa sawa na kushinda uchaguzi katika eneo ambalo chama hicho kina wafuasi wengi.

“Kupata tiketi ya UDA katika mchujo na kuvutia umakini wa Rais ni sawa na kushinda uchaguzi katika eneo ambalo UDA ina nguvu. Haya ni mapambano ya kufa au kupona,” alisema.

Katika ziara yake, Rais Ruto alilazimika mara kadhaa kuwataka wafuasi wa makundi hasimu kudumisha umoja ili mikutano ya maendeleo isigeuke uwanja wa malumbano ya kisiasa.

Pia alikumbana na malalamishi kuhusu utendaji wa baadhi ya viongozi wa maeneo ya Elgeyo Marakwet na Nandi, ambapo wakazi walihoji rekodi zao za maendeleo.

Akijaribu kutuliza hali, Rais aliwataka wagombea na wafuasi wao kubaki ndani ya UDA na serikali jumuishi hadi wakati wa kuchagua viongozi utakapofika.

“Mnajua la kufanya kwa kura zenu. Subirini wakati huo, kisha mfanye uamuzi wenu. Kwa sasa, tuungane ndani ya UDA na serikali jumuishi,” alisema, huku akisisitiza kaulimbiu mpya ya chama, Usawa ni Sawa.

Rais pia aliwataka wapiga kura kuchagua viongozi kwa kuzingatia rekodi zao za maendeleo, sera na ahadi zao badala ya kufuata ushawishi wa kisiasa pekee.

Alisema ana imani kuwa serikali yake imefanya mengi katika miaka minne iliyopita na akapuuza uwezekano wa upinzani kumshinda mwaka 2027.