Afya na JamiiPambo

Ilani kuhusu baadhi ya vyakula na afya ya akili kwa matineja

Na MARY WANGARI October 25th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

UJAUZITO NA UZAZI

IWAPO wewe ni mzazi wa vijana barobaro, basi utahitajika kuwa mwangalifu zaidi kuhusu uteuzi wao wa chakula ili kulinda afya yao ya akili. 

Wataalam wanatahadharisha kuwa chaguo la vyakula kwa vijana chipukizi linaweza kuwa na madhara zaidi ya afya yao kimwili. 

Chaguo la chakula na ulaji wa sukari limehusishwa na kuzuka baadaye kwa matatizo ya afya ya akili hususan wasiwasi uliokithiri na unyogovu, kulingana na utafiti mpya. 

Udadisi huo uliashiria kwamba kula kiasi cha ziada cha aina yoyote ya matunda kila siku kunapunguza dalili za unyogovu kwa asilimia 13 na wasiwasi uliokithiri kwa asilimia saba. 

Kiasi cha jumla cha ulaji wa matunda kilihusisha kula matunda mara mbili au tatu kwa siku katika kipindi cha utafiti huo ulioshirikisha vijana barobaro 6,537 kutoka shule 71 za sekondari Uingereza na Australia. 

Washiriki wenye umri wa miaka 12.5 kwa jumla kutoka Gredi 7- Gredi 10 waliangaziwa kwa miaka minne hadi uchunguzi huo ulipokamilika, 

Kunywa vinywaji vilivyoongezwa sukari ikiwemo soda, sharubati na vinywaji vya spoti kulihusishwa na ongezeko la unyogovu na wasiwasi. 

Uhusiano kuhusu vinwaji vyenye sukari uligunduliwa miongoni mwa vijana chipukizi wavulana kwa wasichana, japo wavulana walionyesha viwango vya juu zaidi hasa wasiwasi uliokithiri. 

“Sekondari ni kipindi ambapo vijana chipukizi huanza kupata uhuru zaidi kuhusu wanachokula na kunywa, wakati huo pia, matatizo mengi ya afya ya akili huanza kuchipuka,” walifafanua watafiti. 

“Hatusemi kula tufaha kutazuia unyogovu, au kwama kunywa soda kutasababisha wasiwasi – afya ya akili inahusu zaidi ya hayo. Lakini unachokula ni sehemu moja ya maisha ya kijana inayoweza kubadilishwa hivyo kufanya matokeo haya kuwa muhimu kwa mtazamo wa kinga.” 

Ni rahisi kufikiria chakula na lishebora kama zinazohusu afya ya mwili lakini utafiti huu unaongeza ushahidi kwamba wanachokula vijana ni muhimu vilevile kwa afya yao ya akili, wanasema wataalam. 

Wanasisitiza umuhimu wa kuelewa kinachoongoza maamuzi bora ya chakula kwa vijana barobaro na kupatia kipaumbele lishebora kiafya ili kulinda afya yao ya akili. 

“Shule, familia na serikali wote wana jukumu la kutekeleza kusaidia tabia inayozingatia afya na afya bora ya akili kwa vijana.”