Mateso ya kustaafu:Yafichuliwa wastaafu 80,000 wanaishi kwa pensheni ya Sh4,000 kwa mwezi
ZAIDI ya wafanyakazi 80,000 waliostaafu serikalini wanapokea pensheni ya Sh4,000 pekee kwa mwezi, huku wabunge wakishinikiza serikali kuongeza malipo hayo ili kukabiliana na gharama ya maisha inayozidi kupanda.
Kamati ya Bunge kuhusu Maombi ya Umma imeitaka Wizara ya Fedha na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kuwasilisha ndani ya miezi miwili ripoti kuhusu fedha zinazohitajika kuongeza pensheni ya wastaafu 319,207.
Hatua hiyo inafuatia malalamishi ya wastaafu kuwa wamekuwa wakilipwa viwango vya chini kwa miaka mingi licha ya kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma muhimu.
Malalamishi hayo yaliwasilishwa bungeni na Chama cha Kitaifa cha Wastaafu wa Utumishi wa Umma (KNAPS), tawi la Kericho, kinachowakilisha wastaafu kote nchini.
Chama hicho kinasema takriban asilimia 25 ya wanachama wake, sawa na watu 80,000, hupokea chini ya Sh4,000 kila mwezi, kiasi ambacho hakiwezi kukidhi mahitaji yao ya kimsingi.
Wastaafu hao wanataka mifumo ya zamani ya pensheni isiyokuwa na michango ya wafanyakazi iunganishwe na mfumo wa sasa wa Public Service Superannuation Scheme (PSSS), ambao wanadai una manufaa bora.
Pia wanataka pensheni zao ziongezwe mara kwa mara ili kuendana na kupanda kwa gharama ya maisha, pamoja na sheria kurekebishwa ili kuwalinda wao na familia zao.
Katika ripoti iliyowasilishwa Bungeni Septemba 30, kamati ilipendekeza Wizara ya Fedha kushirikiana na SRC kufanya tathmini ya gharama za pensheni kila baada ya miaka mitatu.
Tathmini ya kwanza inapaswa kukamilika kufikia Desemba 31, 2026.
Hata hivyo, pendekezo la kuunganisha mifumo hiyo limekabiliwa na upinzani kutoka kwa taasisi mbalimbali za serikali kutokana na gharama kubwa inayoweza kuhusika.
Mamlaka ya Kusimamia Manufaa ya Wastaafu (RBA) iliambia kamati kuwa kuunganisha mifumo hiyo kutahitaji serikali kwanza kulipa madeni ya pensheni yaliyolimbikiza, yanayokadiriwa kuzidi Sh1 trilioni.
Mkurugenzi Mkuu wa RBA Charles Machira alisema tathmini ya Wizarea ya Fedha ya Juni 2024 ilionyesha kuwa madeni hayo yalikuwa yamezidi Sh1 trilioni.
Wizara inasema inatumia takriban Sh7.8 bilioni kila mwezi kulipa wastaafu 319,207, sawa na Sh93.7 bilioni kwa mwaka.
Mfumo wa zamani haukuwa ukikata michango kutoka mishahara ya wafanyakazi. Badala yake, pensheni ziliamuliwa kwa mujibu wa sheria zilizokuwepo wakati huo.
Mfumo mpya ulioanza Januari 2021 unawataka wafanyakazi kuchangia asilimia 7.5 ya mishahara yao kila mwezi, huku serikali ikiongeza kiasi sawa.
Kufikia Juni 2026, wafanyakazi 529,635 walikuwa wamejiunga na mfumo huo, wakiwa wameweka akiba ya Sh343.75 bilioni.
SRC imesema ongezeko lolote la pensheni lazima lizingatie uwezo wa kifedha wa serikali.
Idara ya Utumishi wa Umma pia imeonya kuwa kuongeza pensheni kutaleta mzigo wa muda mrefu kwa serikali, hivyo ni lazima kuhakikisha malipo hayo yanaweza kudumishwa.