Jithamini mwanamume, usirudie mwanamke aliyekusaliti
Katika maisha, mwanaume anahitaji kuwa na misimamo, kujithamini na kujua namna ya kushughulika na watu wanaomzunguka. Mafanikio hayaji kwa bahati pekee, bali pia yanahitaji nidhamu, bidii na uwezo wa kufanya maamuzi yanayofaa.
Mtaalamu wa masuala ya ustawi wa maisha Nelson Kawei anaorodhesha mambo kadhaa ambayo yanaweza kumsaidia mwanaume kujijenga na kuboresha maisha yake.
Usirudie mwanamke aliyekusaliti
Mapenzi yanahitaji uaminifu. Ikiwa mtu amekusaliti na kuvunja imani yako, usikimbilie kurudiana naye bila kutathmini kilichotokea na kama uhusiano huo unaweza kujengwa upya.
Usikubali kudharauliwa
Jithamini na weka mipaka katika mahusiano yako. Heshima inapaswa kuwa ya pande zote, na si lazima uvumilie matusi au unyanyasaji ili kudumisha uhusiano.
Simama unapomsalimia mtu kwa mkono
Kusimama unapopeana mikono kunaweza kuonyesha adabu na heshima, hasa unapokutana na mtu katika mazingira rasmi.
Usiishi kwa kutaka kuwafurahisha watu
Usitumie pesa ambazo huna ili kuonekana tajiri au kufurahisha marafiki. Ishi kulingana na uwezo wako na uweke kipaumbele katika mahitaji muhimu.
Usile kipande cha mwisho cha chakula ambacho hukununua
Zingatia hisia zao. Kutokula kilichobaki ni ishara ya kujali na kushirikiana.
Daima jitahidi kuwa bora zaidi
Weka malengo ya kuboresha maisha yako kielimu, kikazi, kifedha na kibinafsi. Usiridhike na hali uliyonayo ikiwa unaweza kufanya zaidi.
Walinde walio nyuma yako na uwaheshimu walio kando yako
Wasaidie wanaokutegemea na uwaheshimu marafiki, wafanyakazi wenzako na watu wanaosafiri nawe katika safari ya maisha.
Fikiri kabla ya kujibu swali
Unapoulizwa swali, tulia kwa sekunde chache kabla ya kujibu. Hilo linaweza kukusaidia kupanga mawazo na kuepuka kusema jambo kwa pupa.
Usilazimishe mahusiano
Mapenzi yanahitaji ridhaa na juhudi za pande zote. Usijishushe kwa kuomba mtu akupende au abaki nawe ikiwa hataki kuwa katika uhusiano huo.
Fanya mazoezi mara kwa mara
Tenga muda wa kufanya mazoezi angalau mara nne kwa wiki, kulingana na afya na uwezo wako. Mazoezi yanaweza kusaidia kuimarisha mwili na kuboresha ustawi wa jumla.
Usijilazimishe kwenda mahali ambapo hujaalikwa
Ikiwa marafiki wamepanga shughuli bila kukualika, usijilazimishe kujiunga nao. Heshimu mipaka yao na tafuta shughuli zinazokufurahisha.
Beba kiasi cha pesa taslimu
Ingawa malipo ya simu na kadi yamerahisisha maisha, kuwa na kiasi kidogo cha pesa taslimu kunaweza kukusaidia pale njia hizo zinapokosa kufanya kazi.
Vaa vizuri kulingana na shughuli
Huhitaji nguo za bei ghali ili uonekane nadhifu. Chagua mavazi safi, yanayokutosha vizuri na yanayofaa tukio husika.
Sikiliza kwa makini unapozungumza na watu
Tikisa kichwa kuonyesha kuwa unafuatilia mazungumzo na tazama mtu usoni kwa namna inayofaa. Hata hivyo, epuka kumkodolea macho kiasi cha kumfanya akose raha.
Tafuta njia mbalimbali za kupata mapato
Usitegemee kwa chanzo kimoja cha mapato ikiwa una nafasi ya kufanya zaidi. Unaweza kujifunza ujuzi mpya, kuanzisha biashara ndogo au kufanya kazi ya ziada kulingana na uwezo wako.
Kujiheshimu, afafanua Kawei, si kuwadharau wengine au kujifanya mkamilifu. Ni kujua thamani yako, kuheshimu watu, kutumia pesa kwa busara na kujitahidi kuboresha maisha yako kila siku.