Pambo

SHERIA: Hauwezi kutunzwa milele na mchumba wako mkitalikiana

Na BENSON MATHEKA November 1st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

Je, mtu aliyepewa posho ya matunzo na mahakama ana haki ya kuendelea kupokea fedha hizo maisha yake yote? Sheria ya Ndoa ya Kenya inaeleza kuwa malipo hayo yanaweza kukoma kutokana na mambo fulani.

Chini ya kifungu cha 78, agizo la matunzo ya mwanandoa linaweza kukoma katika hali tofauti, kutegemea namna lilivyowekwa na mazingira ya wahusika.

Kwa mfano, ikiwa agizo halikuwekewa dhamana, linaweza kukoma baada ya kifo cha aliyekuwa akipokea matunzo. Ikiwa matunzo yaliwekewa dhamana, agizo hilo hukoma baada ya kifo cha anayelipwa.

Sheria pia inasema kuwa agizo la matunzo linaweza kukoma ikiwa mtu anayepokea fedha hizo baadaye ataweza kujikimu mwenyewe.

Hii ina maana kuwa hali ya kifedha ya anayelipwa posho ni muhimu katika kuamua iwapo malipo yanapaswa kuendelea. Mtu ambaye awali alihitaji msaada wa kifedha anaweza baadaye kupata uwezo wa kujitegemea.

Kifungu cha 79 kinaongeza kuwa agizo la matunzo hukoma anayelipwa anapoingia katika ndoa nyingine.

Hata hivyo, sheria haimaanishi kuwa anayelipa anaweza kusitisha malipo kwa uamuzi wake mwenyewe kila anapohisi kuwa hali imebadilika. Kifungu cha 80 kinapatia mahakama mamlaka ya kubadilisha au kufuta agizo lililopo ikiwa imeridhika kuwa lilitokana na taarifa zisizo za kweli au kosa la ukweli, au kumekuwa na mabadiliko makubwa ya hali tangu agizo lilipotolewa.

Mahakama pia inaweza kubadilisha masharti ya makubaliano ya matunzo kati ya wanandoa iwapo kutakuwa na mabadiliko makubwa ya mazingira.

Kwa upande mwingine, sheria inalinda fedha za matunzo dhidi ya madai ya madeni. Kifungu cha 81 kinasema kuwa fedha hizo haziwezi kuhamishwa kwa mtu mwingine wala kutwaliwa ili kulipia deni la anayelipwa.

Kifungu cha 82 kinaweka muda wa miaka mitatu wa kuanzisha kesi ya kudai kila malipo ya matunzo yaliyochelewa. Baada ya muda huo, malipo husika hayawezi kudaiwa kupitia kesi mpya.

Sheria pia inaruhusu malimbikizi yanayostahili kudaiwa kuwa deni la kiraia, yakiwemo katika mazingira fulani baada ya kifo cha mhusika.

Kwa hivyo, posho ya matunzo si malipo yanayoendelea bila kujali mazingira. Sheria inaweka masharti ya kukomeshwa, kubadilishwa au kufutwa kwa agizo la kuyalipa. Hata hivyo, uamuzi wa kusitisha au kubadilisha agizo kwa sababu ya mabadiliko ya hali unapaswa kufuata utaratibu wa mahakama.