Wabunge walivyokataa mapendekezo ya muafaka wa Ruto na Raila
WABUNGE wa Bunge la Kitaifa wamekataa marekebisho yaliyopendekezwa na Seneti kuhusu kuhesabu na kupeperusha matokeo ya uchaguzi wa urais kwa njia ya kielektroniki, hatua iliyozua malumbano bungeni.
Mapendekezo hayo yalitokana na mazungumzo ya kisiasa kati ya timu za Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, yakilenga kuzuia ucheleweshaji wa kutangaza mshindi wa urais na kuimarisha uwazi katika uchaguzi.
Seneti ilikuwa imependekeza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itume matokeo ya kila kituo cha kupigia kura ndani ya saa mbili baada ya kutangazwa. Matokeo hayo yangetumwa kwa vituo vya kujumlisha kura vya maeneo bunge, kituo cha kitaifa, wagombeaji, maajenti wao na waangalizi wa uchaguzi.
Pia, mapendekezo hayo yalitaka IEBC kuanzisha mfumo wa kurusha moja kwa moja matokeo ya urais yanayotangazwa katika vituo vya kujumlisha kura vya maeneo bunge, ikiwemo kura za Wakenya wanaoishi ughaibuni.
Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, alikuwa amependekeza matokeo hayo yaonyeshwe moja kwa moja ili wananchi waweze kuyafuatilia na kuyalinganisha na matokeo ya mwisho.
Hata hivyo, wakati wa kujadili Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi 2024 ulioanzia Seneti , Mbunge wa Homa Bay Town Peter Kaluma, akiungwa mkono na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah, alifanikiwa kushawishi Bunge kufuta mapendekezo hayo.
Hatua hiyo iliwakasirisha baadhi ya wabunge waliotaka sheria ibadilishwe ili kuondoa utata kuhusu uwasilishaji wa matokeo.
Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alihoji kwa nini Bunge lilikuwa likifuta mapendekezo yaliyotokana na mazungumzo ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO).
Alisema Kenya haipaswi kusubiri siku saba au nane kutangazwa kwa matokeo ya urais wakati teknolojia inaweza kusaidia kuyawasilisha haraka.
Mzozo huo unatokana pia na uamuzi wa Mahakama Kuu wa Aprili 6, 2026, ambapo Jaji Chacha Mwita alitangaza kifungu cha sheria kilichoruhusu matokeo kurushwa moja kwa moja kwa madhumuni ya kuwafahamisha wananchi kuwa kinyume cha Katiba.
Mahakama ilisema matokeo yanayotangazwa katika vituo vya kupigia kura ndiyo msingi wa matokeo ya mwisho na hayawezi kuchukuliwa kuwa taarifa za kuwafahamisha wananchi pekee.
Hata hivyo, Bunge lilisema halijapiga marufuku kupeperushwa kwa matokeo moja kwa moja, bali limehifadhi utaratibu uliopo katika Sheria ya Uchaguzi.
Wabunge pia walisema mabadiliko makubwa ya sheria za uchaguzi miezi michache kabla ya uchaguzi wa 2027 yanaweza kukiuka mapendekezo ya ripoti ya Kriegler, iliyotaka sheria hizo zisibadilishwe ndani ya mwaka mmoja kabla ya uchaguzi.