Polisi wadai wakili Abshir Abdi aliyetekwa nyara anahusika na genge la ulaghai
POLISI wanadai kuwa wakili Abshir Ahmedsadak Abdi, ambaye alitoweka baada ya kutekwa nyara na watu wenye silaha jijini Nairobi, huenda alikuwa sehemu ya mtandao wa ulaghai ambapo watu hukamatwa kwa lazima kisha kulazimishwa kutoa pesa.
Hata hivyo, maafisa wa usalama waliohojiwa mahakamani walisema wakili huyo hayuko mikononi mwa polisi na uchunguzi unaendelea kubaini aliko.
Afisa Mkuu wa Polisi Vitalis Kimutai, anayesimamia kitengo cha kupambana na ugaidi jijini Nairobi, aliambia Mahakama Kuu ya Milimani kuwa Abdi alikuwa amechunguzwa awali kuhusu madai ya utekaji nyara na ulaghai.
Alidai mtandao huo ulihusisha maafisa kutoka vituo vya polisi vya Pangani, Shauri Moyo, Airbase, Eastleigh North na California, ambapo watu waliokataa kutoa pesa walikamatwa na kushtakiwa.
Jaji Alexander Muteti alipouliza kama polisi walikuwa wakikamata watu kwa mashtaka ya kubuni baada ya kukataa kulipa pesa, Kimutai alijibu: “Ndiyo, hilo ndilo hasa nililosema.”
Alisema Abdi alikamatwa Agosti 13 na Oktoba 24, 2025, na kufikishwa katika Mahakama za Kahawa. Hata hivyo, aliachiliwa kwa dhamana ya polisi baada ya waendesha mashtaka kutounga mkono ombi la kumzuilia.
Wakati huo huo, familia ya wakili huyo inadai alipokea vitisho kutoka kwa watu wanaohusishwa na Idara ya Ujasusi (NIS), DCI na kitengo cha kupambana na ugaidi, wakimtaka ajiondoe katika kesi ya jinai ambako alikuwa shahidi.
Ndugu yake Zakaria Abshir alisema Abdi alitekwa alfajiri ya Novemba 1, 2026, akiwa ya Muchai Road, karibu na Ngong Road, na watu waliokuwa wamejihami.
Alisema picha za kamera za usalama zilionyesha watu watatu waliokuwa na silaha wakimkamata mwanamume na kumuingiza kwa nguvu kwenye gari.
Polisi walisema hawamzuilii katika kituo chochote nchini. Gari lake aina ya Toyota Premio lilipelekwa Kituo cha Polisi cha Kilimani kwa uchunguzi wa alama za vidole.
Familia inataka mahakama iagize idara za usalama kumwasilisha Abdi akiwa hai au maiti, huku ikiomba uchunguzi huru kuhusu kutoweka kwake.
Kesi hiyo bado inasubiri uamuzi wa mahakama.