Makala

TAHARIRI: Ukimwi bado hauna tiba japo kuna tumaini

March 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA MHARIRI

WANASAYANSI hatimaye wamedokeza kuwa huenda tiba ya maradhi ya Ukimwi ikapatikana baada ya kufanya majaribio kwa zaidi ya miongo miwili.

Hii ni baada ya madaktari kutoka Chuo Kikuu cha London kufanikiwa kumponya mgonjwa aliyekuwa na virusi vya Ukimwi vinavyosababisha maradhi ya Ukimwi.

Huyo ni mgonjwa wa pili ambaye wanasayansi wanaamini kwamba alitibiwa kutokana na maradhi ya Ukimwi.

Uvumbuzi huo ni habari njema kote duniani na huenda ukawa ushindi mkubwa dhidi ya maradhi ya Ukimwi yanayoangamiza zaidi ya watu 20 kila siku humu nchini.

Habari ya uponyaji wa mgonjwa huyo wa Ukimwi huenda zikafasiriwa visivyo na wengi kwamba dawa ya Ukimwi imepatikana.

Ukweli ni kwamba, dawa ya Ukimwi bado haijapatikana na wanasayansi wangali wanaendelea na utafiti.

Mgonjwa huyo alipatikana na maradhi hayo mnamo 2003 na kuanzia wakati huo amekuwa akitbiwa na wataalamu hao. Hiyo imaanisha kwamba kwa sasa matibabu hayo ni ghali mno.

Hivyo itachukua miaka kadhaa kabla ya tiba hiyo kuanza kutumika na kuwafaa zaidi ya wagonjwa 37 milioni wanaoishi na virusi vya HIV kote duniani. Humu nchini, takribani watu 1.5 milioni wanaishi na virusi vya Ukimwi.

Japo Kenya imepiga hatua katika kukabiliana na maafa yanayotokana na Ukimwi, ripoti ya mwaka jana kuhusu Hali ya Kiuchumi iliyoandaliwa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) inaonyesha kuwa maradhi hayo yangali tishio.

Ripoti hiyo ilionyesha kuwa Ukimwi uko katika nafasi ya nne kwa kuua idadi kubwa ya watu humu nchini nyuma ya malaria, nimonia na saratani.

Kwa mfano, mnamo 2015 watu 11,131, ambao ni sawa na watu 30 kwa siku, walifariki kutokana na maradhi ya Ukimwi.

Watu 9471 na 8,758 walifariki kwa Ukimwi mnamo 2016 na 2017.

Kupungua huko kunatokana na juhudi za serikali kuhimiza matumizi ya kinga kama vile mpira ya kondomu.

Ugonjwa wa Ukimwi bado hauna tiba hivyo, kuna haja ya kuendelea kutumia kinga zilizopo kama kawaida.