• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
Wakazi 2,221 waililia mahakama iwape hatimiliki ya shamba la Sh1 bilioni

Wakazi 2,221 waililia mahakama iwape hatimiliki ya shamba la Sh1 bilioni

Na RICHARD MUNGUTI

WANAKIJIJI 2,221 waliomshtaki mkurugenzi mkuu wa shirika la kustawisha makazi ya wakazi wa mitaa ya mabanda mijini Bi Jane Weru Alhamisi waliomba mahakama kuu imshurutishe awape hati ya umiliki wa shamba la ekari 23 lenye thamani ya Sh1 bilioni waliyonununua miaka 12 iliyopita.

Wakazi hawa walimweleza Jaji Elijah Obaga kwamba walinunua shamba hilo kutoka kwa kampuni ya Mill White Limited kwa thamani ya Sh81 milioni mwaka 2009.

Tangu wanunue shamba hilo, hawajapewa hatimiliki. “Uchunguzi tuliofanya ulibaini Bi Weru alipewa hatimiliki na Benki ya Ecobank pamoja na taarifa ya akaunti ya kampuni hii,” Jaji Obaga alifahamishwa.

Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Obaga, Bi Weru alikiri alipokea pesa kutoka kwa wakazi hawa aliowasaidia kununua shamba hili.

Bi Weru aliyekuwa amependekezwa na Gavana Mike Sonko kuwa mmoja wa kuwania wadhifa wa Naibu wa Gavana alishindwa kueleza sababu ya kutoandikisha shamba hilo kwa jina la Mukuru Makao Bora Trust iliyoundwa na walalamishi 2009.

Bi Weru alisema alipokea ruzuku ya Sh24 milioni kutoka kwa wakfu wa Bill and Melida Gates na kuweka katika benki ya Ecobank iliyowapa wanakijiji hawa mkopo wa Sh55 milioni kununua shamba hilo.

“Je, walalamishi walimaliza kulipa mkopo huo?” Wakili Abubakar Ramadhan anayewawakilisha walalamishi hawa alimwuliza Bi Weru.

“Ndio, walimaliza kulipa mkopo huo 2013. Walimaliza kuulipa kwa miezi 19,” alijibu Bi Weru huku akiongeza, “Nilipewa hatimiliki ya shamba hili , taarifa ya akaunti yao katika benki ya Ecobank.”

Mkurugenzi huyo alidai sababu ya kutowapa walalamishi hati ya umiliki wa shamba hilo ni kuwa anawadai Sh24 milioni lakini hakuwasilisha ushahidi kuthibitisha alikuwa anawadai.

Na wakati huo huo Bi Weru ambaye pia ni wakili alikiri kwamba ameshtakiwa na wanachama wengine wa kikundi cha Machakos kwa kutowapa hatimiliki ya shamba alilowasaidia kununua.

Bi Weru ni mkurugenzi mkuu wa Muungano wa Wanavijiji Akiba Mashinani Trust (AMT).

Mkurugenzi huyo alikanusha ushahidi kwamba amekuwa akiweka hati miliki za mashamba ya wakazi ya wanavijiji “ kupokea pesa kutoka kwa mashirika ya kimataifa.”

Bi Jane Weru akijitetea mahakamani Machi 7, 2019. Picha/ Richard Munguti

Bw Ramadhan aliwasilisha ushahidi kwamba Bi Weru ameendelea kutumia akaunti ya AMT kupokea mamilioni ya pesa katika benki ta Ecobank licha ya madai akaunti hiyo ilikuwa imefungwa.

Mkurugenzi huyo alijipata taabani aliposhindwa kueleza ikiwa aliungana na baadhi ya wanachama wa Mukuru Makao Bora kuhujumu utendakazi wake.

Bi Weru alisema Mukuru makao bora yako na vikundi 32 na kwamba kikundi cha Quarry kilikuwa kimekusanya Sh10milioni kwa ajili ya ununuzi wa shamba hilo.

“Wewe na mmoja wa wanachama walioasi Bw John Mbatia ni kitu kimoja. Mnawakilishwa na wakili mmoja Bw Timothy Brant,” Bw Ramadhan alimwuliza Bi Weru.

Bi Weru alikanusha madai hayo na kusema kila mmoja anatetewa na wakili Brant kwa mambo yake.

Akijibu maswali Bi Weru alisema kuwa amekuwa akipokea barua kutoka kwa wanachama wa Mukuru Makao Bora na kusema miongoni mwao ni Mbatia aliyedai “alikuwa amemweleza asitoe hati miliki kwa kundi linaloongozwa na Bw Robert Okwoyo Mironga.”

Mkurugenzi huyo alikana kuwa anatumia makundi ya wanakijiji kujipatia pesa za misaada kutoka kwa wafadhili Ulaya.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mkurugenzi huyo alikuwa anapokea misaada kwa niaba ya wakazi wa mitaa ya mabanda kutoka Wakfu wa Rockefeller wa Afrika kusini na Bill and Melida Gates.

Ijapokuwa alikana, mkurugenzi huyo alionyeshwa ripoti ya benki ya Ecobank kuthibitisha alikuwa akipokea mamilioni ya pesa licha ya kuwaeleza wanakijiji hao akaonti yao katika benki hiyo ilikuwa imefungwa.

Kesi itaendekea kusikizwa Mei 13.

You can share this post!

TAHARIRI: Ni wazi hatua za ugatuzi bado hafifu

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Maendeleo ya Kiswahili katika...

adminleo