• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
JAMVI: Ishara zote zaonyesha huenda Uhuru asimuunge mkono Ruto 2022

JAMVI: Ishara zote zaonyesha huenda Uhuru asimuunge mkono Ruto 2022

Na WANDERI KAMAU

KUONGEZEKA kwa malumbano ya kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kundi la wabunge la ‘Tanga Tanga’ kumeibua taswira ya wazi kwamba huenda Rais Kenyatta akakosa kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais mnamo 2022.

Wabunge hao, ambao wanamuunga mkono Dkt Ruto wamekaidi agizo la Rais Kenyatta kutofanya kampeni zozote, kwani licha ya agizo hilo, limekuwa likiendeleza semi zao katika majukwaa mbalimbali, likisisitiza kwamba ukanda wa Mlima Kenya utamuunga mkono Bw Ruto.

Upeo wa uhasama huo ulidhihirika mnamo Jumatatu, baada ya Rais Kenyatta kuondoka jukwaani wakati mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro, alipoanza kuwahutubia waombolezaji waliohudhuria mazishi ya mfanyabiashara Thayu Kamau Kabugi katika Kaunti ya Murang’a.

Duru zilieleza kwamba, Rais Kenyatta aliondoka katika kiti chake na kurejea baada ya mbunge huyo kumaliza hotuba yake. Bw Nyoro ni miongoni mwa wabunge kadhaa wa Kati ambao ni wanachana wa kundi la ‘Tanga Tanga.’

Wengine wanaohusishwa nalo ni mbunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), Kimani Ichug’wa (Kikuyu), Gavana Mwangj wa Iria (Murang’a), Gavana Ferdinard Waititu (Kiambu), Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a) kati ya wengine.

Kwa kutumia lugha ya Gikuyu, Rais aliwakaripia vikali wabunge hao, akisema kwamba aliachana nao, kwani wanaendeleza siasa hata wakati wananchi wanahitaji kufanyiwa kazi.

“Nii ni ndatiganire nao. Matiindaga makiriunga guku magiika kampiini haandu ha kurutira wiira muingi. Nii ndameerire matikaandange,” akasema Bw Kenyatta. (Mimi niliachana nao. Wao hushinda wakienda katika majukwaa mbalimbali kufanya kampeni badala ya kuwatumikia wananchi. Mimi niliwaambia wasinisumbue).

Na kama kile kinaonekana kumjibu Rais na kumtetea Bw Nyoro, kundi hilo limejitokeza vikali kumtetea mbunge huyo, likisema kwamba wana haki ya kutembea watakako, kwani lengo lao kuu ni kuwatetea watu wao ili kuwaletea maendeleo.

“Kila kiongozi ana haki ya kufanya lolote analohisi kwamba litawafaa watu wake. Tunaegemea mirengo fulani kwa manufaa ya watu wetu, ila si sisi wenyewe. Hakuna mwenye haki ya kumkosoa kiongozi yeyote kwa kutetea maslahi ya watu wake,” akasema Bw Kuria, kwenye kauli iliyoonekana kumlenga Rais Kenyatta.

Kutokana na majibizano hayo, wadadisi wameonya kwamba hizo ni dalili za wazi kwamba uasi huo ni dhihirisho kamili kuwa kundi hilo limo tayari kumfanyia kampeni Dkt Ruto, hata ikiwa Rais Kenyatta hatamuunga mkono.

Kulingana na Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, majibizano hayo ni ishara kwamba kuna tofauti kubwa fiche kati Rais Kenyatta na Dkt Ruto, kwani uasi huo unafasiriwa kama kumkosea heshima Rais.

“Hili ni kundi ambalo linamuunga Bw Ruto. Rais ameagiza likomeshe kampeni za mapema, ila limekataa. Fasiri ya moja kwa moja ni kwamba wanapata baraka zao kutoka kwa Dkt Ruto mwenyewe,” asema mchanganuzi huyo.

Mwezi uliopita, Rais Kenyatta aliwaagiza viongozi wote wa Jubilee kukomesha kampeni za mapema ili kumpa nafasi ya kutimiza Ajenda Nne Kuu za Maendeleo, ila kundi hilo limekuwa likikaidi agizo hilo.

Hata hivyo, mwito wa Rais ulionekana kuzingatiwa na kundi la ‘Kieleweke’ linalojumuisha wanasiasa ambao wanasisitiza kwamba ni mapema kuanza kampeni za 2022, kwani wananchi bado hawajasahau kampeni tata za 2017.

Kundi hilo limekuwa likiongozwa na mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu, anayeonekana kupata uungwaji mkono kutoka kwa wabunge wengi katika kaunti hiyo.

Mgawanyiko huo ulidhihirika wazi majuma mawili yaliyopita, baada ya wabunge wote wa kaunti hiyo kususia hafla iliyoandaliwa na mbunge Rigathi Gachagua wa Mathira, ambapo Dkt Ruto alihudhuria.

Wakili Wahome Gikonyo, ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa, anasema kwamba uasi wa kundi la ‘Tanga Tanga’ ni utabiri wa mapema kwamba huenda Rais Kenyatta asimuunge mkono Dkt Ruto, kwani inavyoonekana ni kuwa kuna mkono wake ndani ya uasi huo.

Mchanganuzi huyo pia anasena kwamba kwa mara ya kwanza, huenda sehemu kubwa ya wapigakura wakazingatia miito ya kundi hilo kwa kumkaidi Rais Kenyatta.

“Uasi huu unazidi kuongezeka kwa kiwango cha kushtua. Hii ni ishara ya mapema kwamba ni mkondo utakaoendelea kudhihirika ielekeapo 2022. Itabidi Rais Kenyatta kuanza mikakati mipya ya kisiasa kulizima, la sivyo huenda likaendelea kupata mpenyo zaidi siku zinavyosonga,” aeleza mchanganuzi huyo.

Baadhi ya wanachama wa kundi hilo hata hivyo wamekuwa wakisisitiza kwamba lengo lao kuu ni kuhakikisha kwamba eneo la Mlima Kenya ‘limerudisha mkono’ kwa Dkt Ruto, kwa kumuunga mkono Rais Kenyatta mnano 2013 na 2017.

Kwa upande wao, wanachama wa kundi la ‘Kieleweke’ wanashikilia kwamba ushawishi wa Rais Kenyatta ungalipo na hakuna yeyote anaweza kuuingilia.

“Rais Kenyatta atabaki kigogo wa kisiasa na kiongozi wa Mlima Kenya. Wakazi wataunga mkono chaguo lake,” asema Bw Wambugu.

You can share this post!

JAMVI: ‘Nyumba ya Jubilee itaporomoka kabla ya...

MWANASIASA NGANGARI: Ushawishi wa Jaramogi Oginga...

adminleo