Wakenya 32 wafariki Ethiopia
BERNADINE MUTANU, WANDERI KAMAU na ANITA CHEPKOECH
WAKENYA 32 waliangamia Jumapili asubuhi nchini Ethiopia, wakati ndege waliyokuwa wakisafiria kuja Nairobi kutoka Addis Ababa, ilipoanguka dakika sita baada ya kupaa angani.
Wakenya hao walikuwa miongoni mwa abiria 157 – abiria 149 na wahudumu wanane – waliofariki katika ajali hiyo viungani mwa jiji la Addis Ababa.
Wengine waliokufa ni kutoka mataifa 33 wakiwemo raia 18 wa Canada, Waethiopia tisa, Wataliano wanane na Waamerika wanane.
Ajali hiyo ilifanyika katika eneo la Bishoftu, karibu maili 40 kaskazini mashariki mwa Addis Ababa na ikasababisha shimo kubwa.
Baadhi ya waliokufa walikuwa wakija nchini kwa ajili ya mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu mazingira unaoanza leo Gigiri.
Kulingana na shirika la ndege la Ethiopian Airlines, ndege hiyo, aina ya Boeing 737 Max Model, ilipoteza mawasiliano mara tu baada ya kupaa angani.
Afisa Mkuu wa Ethiopian Airlines, Tewolde Gebre-Mariam, alisema rubani wa ndege hiyo, Yared Mulugeta, ambaye ni Mkenya aliyezaliwa Ethiopia, na msaidizi wake Ahmednur Mohamednur, walikuwa na ujuzi wa miaka mingi.
Alisema ilikuwa ni mapema sana kujua kiini cha ajali hiyo, lakini CNN ilipomuuliza iwapo walishuku ugaidi akasema kwa sasa hawezi kupuuza uwezekano huo.
Ndege hiyo ilitazamiwa kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi mwendo wa saa nne unusu baada ya kuondoka Addis Ababa saa mbili na dakika thelathini na nane.
Kulingana na shirika la habari la Al Jazeera, ndege hiyo ilinunuliwa Novemba mwaka jana.
Ndege hiyo ilikuwa ya muundo sawa na ile ya Indonesia iliyopata ajali baharini, mara tu baada kupaa katika kisiwa cha Bangka, na kuwaua watu 189 Oktoba mwaka jana.
“Rubani alikuwa ameeleza kupata matatizo akiwa hewani, na alikuwa ameomba kurejea uwanjani na akakubaliwa,” akasema Gebre-Mariam.
Kulingana naye, ndege hiyo ilikuwa mpya na haikuwa na matatizo yoyote ya kimitambo kwani ilifanyiwa ukaguzi mnamo Februari 4 mwaka huu.
Gazeti la New York Times lilisema jana kuwa Amerika itatuma maafisa wanne wa Bodi ya Usalama wa Uchukuzi (NTSB) kusaidiana na maafisa wa Ethiopia katika kuchunguza kiini cha ajali hiyo.
Katika uwanja wa ndege wa JKIA, familia za waliokufa zilikuwa na wakati mgumu kubaini hatima ya wapendwa wao, huku baadhi wakilalamika kwa kukosa kupashwa habari na Ethiopian Airlines.
Akiwahutubia wanahabari jana, Waziri wa Uchukuzi James Macharia, alisema Kenya inashirikiana kwa karibu na Ethiopia.
Hapo jana, Mamlaka ya Kusimamia Viwanja vya Ndege (KCAA) iliweka vituo viwili vya kushughulikia hali za dharura na jamaa za walioathiriwa.
Mamlaka hiyo pia ilitoa nambari ya dharura 0733666066, ili kuwawezesha wananchi kuomba ama kutoa habari zozote la dharura.
Afisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Mohammed ndiyo ilikuwa ya kwanza kutoa taarifa kuhusu ajali hiyo, ikituma rambirambi kwa jamaa za walioathiriwa.
“Tunaeleza masikitiko yetu kutokana na ajali mbaya ya ndege ambayo imetokea. Tunaungana na familia za walioathiriwa katika wakati huu mgumu,” akasema.
Rais Uhuru Kenyatta pia alituma rambirambi zake, akieleza kusikitishwa na ajali hiyo.