Dakika za mwisho kabla ya mkasa wa ndege ya Ethiopia
ALLAN OLINGO Na PETER MBURU
KENYA inaomboleza vikubwa kufuatia ajali ya ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Ethiopia kuelekea Nairobi, ambapo Wakenya 32 waliangamia, kati ya abiria 157 ambao walikuwa katika ndege hiyo.
Iliripotiwa kuwa ndege hiyo ilionyesha dalili za hitilafu dakika mbili tu baada ya kupaa kutoka uwanja wa Kimataifa wa Bole, Jijini Addis Ababa saa 2: 38 (asubuhi) ya Jumapili.
Baada ya mitambo ya usafiri wa ndege kudokeza kuwa haikuwa ikipaa kwa njia inayofaa, hali hiyo inaripotiwa kuendelea kwa dakika tatu na mnamo saa 2:42 asubuhi, ndege hiyo ikakosekana katika mitambo ya kufuatilia usafiri.
Rubani wa ndege hiyo Yared Getachew anaripotiwa kuwa alifahamisha idara ya kufuatilia usafiri wa ndege katika Ethiopia kuwa alikuwa akikumbana na matatizo baada ya kupaa na alitarajiwa kurejea uwanjani Bole kutua tena.
Ndege hiyo ilianguka karibu na kijiji cha Tulu Fara, Bishoftu, takriban kilomita 60 kusini magharibi mwa Addis Ababa na kuua wasafiri wote, marubani wawili na wahudumu sita.
Ndege hiyo ilianza kufanya kazi nchini Ethiopia Oktoba 2018.
Waliokuwa ndani ya ndege hiyo ni raia wa mataifa 33, na kati yao ni Kenya iliyopata pigo kubwa zaidi.
Raia 18 wa Canada waliangamia, tisa wa Ethiopia, kisha Italy, China na Marekani kulingana na wingi wa waliofariki.
Waliokufa walikuwa wa kutoka mataifa 11 ya Afrika na 13 ya bara Uropa.
Wasimamizi wa usafiri wa ndege hiyo walisema bado haijabainika chanzo hasa cha mkasa huo, wakisema uchunguzi umeanzishwa.
“Bado ni mapema sana kubaini kiini cha ajali na uchunguzi zaidi utafanywa kwa ushirikiano na washikadau, ikiwemo kampuni iliyotengeneza ndege hiyo,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji Tewolde Gebremariam.
Aliitaja siku ya ajali hiyo kuwa “ya huzuni sana na ya mkasa.”
Ndege hiyo ilikuwa imesafiri kutoka Johannesburg hadi Addis Ababa, ambapo ilikaa saa tatu kabla ya kupaa tena kuelekea Nairobi, Bw Gebremariam akasema.
Ilikuwa imefanyiwa ukaguzi wa kina mnamo Februari 4, baada ya kununuliwa Oktoba.
Maafisa wa mashirika ya kimataifa kama Katibu Mkuu wa Muungano wa UN Antonio Guterres waliomboleza pamoja na familia za walioangamia.
Waziri wa Uchukuzi humu nchini James Macharia alisema kuwa timu kutoka Kenya ikiongozwa na Katibu katika wizara hiyo Esther Koimett ilitumwa Ethiopia Jumapili kufuatilia hali.
Ajali hiyo ilikuwa ya tatu kama hiyo ikihusisha ndege za Ethiopia, ambapo ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Beirut, Lebanon mnamo 2010 ilianguka punde tu baada ya kupaa na kuangamiza watu 90.
Mnamo 1996 vilevile, moja kati ya ndege za Ethiopia ilitekwa nyara ilipokuwa ikisafiri kutoka Addis Ababa kuelekea Nairobi, kisha ikaanguka katika kisiwa cha Comoros, katika Bahari Hindi na kuua wasafiri 125.