• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
SHANGAZI AKUJIBU: Wangu wa kwanza ameniharibia sifa kwa umbea

SHANGAZI AKUJIBU: Wangu wa kwanza ameniharibia sifa kwa umbea

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Niliachana na kijana mpenzi wangu baada ya kuniacha kwa dharau huku akinisingizia mambo mengi ya uongo. Alidai eti nimekuwa nikigawa ovyo asali mtaani na eti nimepata mimba kadhaa za wanaume tofauti na kuziharibu. Ukweli ni kuwa alikuwa wangu wa kwanza na nilimpenda kwa dhati. Madai yake hayo yameathiri vibaya hisia zangu hata sijui kama nitawahi kumpenda mwanamume mwingine. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Inashangaza kwamba mpenzi wako huyo alikulaumu na kukuacha kwa madai ambayo hayakuwa na msingi. Hatua kama hiyo inaweza tu kutekelezwa na mtu ambaye kwa sababu zake mwenyewe ameamua kujiondoa katika uhusiano kwa vyovyote vile. Kwa sababu hiyo, atakusingizia mambo mabaya zaidi ambayo hayana msamaha bali dawa yake pekee ni kuachana. Bila shaka ametimiza nia yake. Ushauri wangu ni kuwa ujipe moyo kwani huo si mwisho wa maisha. Hatimaye majeraha aliyokusababishia yatapona na umpate mwingine anayestahili penzi lako.

Kuna tatizo shamba likikosa kulimwa?

Vipi shangazi? Tafadhali nahitaji ushauri wako. Nina umri wa miaka 21 na sijawahi kuwa na uhusiano na mwanamume yeyote. Nimekuwa nikipandwa sana na hisia za kushiriki mahaba lakini ninavumulia tu. Je, ninaweza kuwa na tatizo lolote nikikosa huduma hiyo?

Kupitia SMS

Sijawahi kusikia kuhusu matatizo yoyote yanayoweza kumpata mtu kwa kutoshiriki mahaba. Wewe sasa ni mtu mzima na ni jambo la kawaida kuwa na hisia hizo mara kwa mara kwa sababu mwili unahitaji. Hata hivyo, kama hujapata wa kukuhudumia, endelea kuvumilia tu hadi utakapompata.

 

Ni mlafi kupindukia, hata nikiwa naumwa anataka tu!

Shangazi natumai wewe ni mzima. Mimi pia ni mzima, nashukuru. Nina mpenzi tunayependana sana lakini ana tatizo moja tu. Anapenda sana shughuli za chumbani kiasi kwamba hunilazimisha hata nikiwa mgonjwa. Tumegombana mara nyingi kuhusu tabia yake hiyo. Nishauri.

Kupitia SMS

Maelewano na hali ya mtu kumjali mwenzake ni miongoni mwa nguzo kuu za uhusiano wa dhati. Ikifikia hali ya mtu kudai huduma kwa lazima hata mwenzake akiwa mgonjwa, hayo si mapenzi bali ni tamaa na ubinfasi. Bila shaka hayo ndiyo maumbile yake na sidhani atabadilika. Hiyo ina maana kuwa ukimuoa mtaendelea kugombana tu. Kama unahisi huwezi kuvumilia hali hiyo, ni heri umwambie ili muachane.

 

Nilimpigia simu ikapokewa na dada aliyedai ni mkewe

Shikamoo shangazi! Mpenzi wangu alipata kazi mjini miezi miwili iliyopita. Amekuwa akinipigia simu kunihakikishia kuwa bado ananipenda lakini nimepata habari kutoka kwa rafiki yake wa karibu kwamba amemuona mara kadhaa na mwanamke mwingine. Juzi nilimpigia simu ikapokewa na mwanamke aliyedai kuwa mke wake. Nilipomuuliza mpenzi wangu alidai eti wao ni marafiki tu na hajamuoa. Nishauri.

Kupitia SMS

Huhitaji maelezo zaidi kujua kwamba mpenzi wako amepata mwingine. Rafiki yako alikuambia kuwa amekuwa akimwona na mwanamke mwingine na wewe mwenyewe ukathibitisha ulipopiga simu ikapokewa na mwanamke. Isitoshe, mpenzi wako pia amethibitisha ingawa anadai eti huyo ni rafiki tu. Uongo mtupu! Kama bado unafikiria una mpenzi unajidanganya.

 

Nina wanaume wawili, nimeshindwa kuchagua kati yao

Hujambo shangazi? Kuna wanaume wawili ambao wananipenda sana na nimeshindwa nitachagua nani kati yao. Naomba ushauri.

Kupitia SMS

Mpenzi au mume ni chaguo la moyo wa mtu binfasi. Ninaamini unawajua vizuri wawili hao na pia unajua moyoni mwako aina ya mpenzi na mume unayetaka kuwa naye maishani. Tumia kipimo hicho cha moyo wako kuchagua mmoja.

You can share this post!

Chebukati roho mkononi

K’Ogalo yasukumwa hadi mkiani Zamalek ikipepea

adminleo