Habari Mseto

Kanisa ladai upangaji uzazi umelipunguzia waumini

March 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na ALEX NJERU

MAKASISI wa Kanisa Katoliki wamelaumu matumizi ya njia za kisasa za upangaji uzazi kama sababu kuu ya kupungua kwa idadi ya watoto kwenye shule na makanisa katika Kaunti ya Tharaka-Nithi.

Kasisi wa Parokia ya Iruma Gerald Mugendi akizungumza katika kanisa Katoliki la Muthambi alionya kwamba vipindi vya somo la dini vipo hatarini kusitishwa kutokana na ukosefu wa watoto wa kuhudhuria madarasa yanakofundishwa somo hilo.

Alisikitika kwamba hata wanawake wa kanisa katoliki wamezamia upangaji uzazi ilhali wanafahamu fika kwamba hivyo ni kinyume na mafundisho ya kanisa hilo.

“Baadhi ya shule zina watoto wasiozidi watano wanaopokea mafundisho ya dini jambo ambalo limewakosesha kazi walimu wao wa dini,” akalalamika mtumishi huyo wa mungu.

Bw Mugendi alifichua kwamba wanachama wa Muungano wa Wanawake Katoliki wataungana kuzuru makanisa yote ya katoliki katika kaunti hiyo katika kipindi cha majuma matano yajayo kuwahamasisha waumini wao dhidi ya kutopanga uzazi kwa njia za kisasa. Pia aliwataka waumini waliokumbatia upangaji uzazi kusitisha mpango huo na kutubu dhambi hiyo mbele ya mungu.

“Idadi ya chini ya watoto katika kila familia tutakayoruhusu ni watano. Wanawake wote walioweka vifaa vya upangaji uzazi miilini mwao lazima waviondoe na wamwombe mungu msamaha,” akaongeza Bw Mugendi.

Mbunge wa Maara Kareke Mbiuki aliyehudhuria ibada hiyo hata hivyo aliwalaumu wanawake kwa kukumbatia upangaji uzazi bila kuwafahamisha waume wao.

Bw Mbiuki aliwatetea wanaume na akataka wanawake wa kaunti hiyo kujifungua watoto wengi ili kuongeza idadi yao.

“Wanaume hawana hatia. Wakati mwingine wake zetu hupanga uzazi bila ufahamu wetu,” akasema Bw Mbiuki.