• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
AKILIMALI: Mhandisi mkulima hodari wa nyanya

AKILIMALI: Mhandisi mkulima hodari wa nyanya

NA RICHARD MAOSI

Iwapo unataka kuanziasha mradi wa kukuza nyanya kwa ajili ya mauzo au matumizi ya nyumbani, mambo kadhaa yanahitajika kuzingatiwa.

Kwanza mkulima mwenye nia ya kuwekeza katika mradi wa nyanya, awe mkabala na sehemu yenye maji ya kutosha au chemichemi.

Hii inamaanisha kwamba mimea ya nyanya hunyunyiziwa maji, mbali na kupuliziwa dawa ili kuzuia mkurupuko wa maradhi kama vile bacteria wilt na Early Blight.

Pamoja na hayo nzi weupe wanaojificha chini ya majani ya mimea, aghalabu wanapendelea kula mashina na kunyonya majimaji ya virutubishi muhimu.

Ni wajibu wa mkulima kupalilia shamba mapema, na atumie mbegu zilizoidhinishwa na serikali ili kuzuia athari ya majani kutoboka wakati yanapokua.

Akilimali ilifanikiwa kupatana na Ayub Otieno, mkulima chipukizi kutoka eneo la Modern kilomita 6 kutoka mjini Nakuru.

Akiwa mtaalamu wa mitambo ya kompyuta kutoka Chuo Kikuu Cha KCA, aliamua kuzamia kilimo ili kujipatia ujuzi na mapato ya ziada.

Alitaka kuzima kasumba ambayo imekuwa ikienea miongoni mwa vijana kwa muda mrefu, kuhusu ukosefu wa ajira.

Anasema amekuwa akikuza nyanya kuanzia 2015, kupitia udhamini wa mlezi wake Penina Njenga, aliyemkabidhi akiba kidogo kujiajiri.

Japo ni gharama kukuza nyanya ndani ya kitalu , anaamini mstawishaji anaweza kuvuna hadi takriban Sh350,000.

.Ayub Otieno akifurahia baadhi ya mavuno alliyopata msimu uliopita. Picha/Richard Maosi

Ayub alitufichulia kwamba amekuwa akiongezea huduma za mtaalamu wa mimea , kupaisha mradi wenyewe katika hatua nyingine

“Wataalamu husaidia kutoa ushauri wa kitaaluma mbali na kukagua mimea moja kwa moja endapo itahitajika,”alisema

Kabla ya kukuza nyanya alihakikisha hapakuwa na mimea ambayo imewahi kukuzwa hapo kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

”Udongo uwe safi na laini, na endapo kuna mimea iliyokuwa imepandwa katika eneo hilo siku za mbeleni, mkulima apatie shamba lake miezi mitatu hivi ili kuondoa asidi zilizokolea,” aliongezea

Udongo usiwe ni ule wa kushikamana kama wa mfinyanzi, na uchachu (pH) wa udongo uwe kati ya 6.0-7.5.

Ayub anasema alinunua mbegu kulingana na ukubwa wa shamba la kitalu, ambalo ni nafasi ya mita 20 kwa 60.

Alipalilia kwa wakati na kusawazisha kiwango cha asidi mchangani, kwa kutengeneza njia za kuondoa maji yanayosimama shambani hasa msimu wa mvua .

Alizuia msongamano wa mbegu katika sehemu moja kwa kuzipanda ndani ya mashimo akisema ingeepushia mimea , kushindania virutubisho ambavyo ni haba.

Ikumbukwe nyanya zikiwa changa, zinahitaji joto la kutosha ndiposa anashauri mkulima azifunike vizuri kwa mchanga pindi tu baada ya kuzipanda .

Katika eneo lenye mwangaza wa kutosha,kutoka kwenye mmea mmoja hadi mwingine mkulima azingatie urefu wa sentimita 50.Hapa nyanya hukomaa haraka.

Apulizie dawa shamba lake na kuongeza samadi ,pia anaweza kuchanganya mbegu pamoja na dawa za kukabili magugu.

Inahimizwa awekee mimea yake paa dogo, ili kuikinga dhidi ya mvua kali pamoja na upepo, unaoweza kuvunja mashina endapo kilimo ni katika sehemu wazi.

Hii ni kabla ya kusafirisha miche ya nyanya ndani ya kitalu kwa shughuli maalum za ustawishaji.

Ayub anatumia aina ya mbegu za nyanya zinazofahamika kama F1,aidha ameweka tanki ya maji yenye lita 2000 kunyunyiza.

F1 ni nyanya zenye umbo la kuvutia,hufanya vyema katika eneo lililo wazi au ndani ya kitalu.

Anasema nyanya za F1, zina uwezo wa kukabiliana na shinikizo la maradhi na vidudu wanaoweza kunyemelea matawi yanayowanda na kutanua vizuri.

Ndani ya kitalu hukomaa kati ya siku 60-75 , uvunaji huendelea hadi miezi sita mfululizo bila kukatiza mazao.

Baada ya kuchimba mashimo Ayub huweka mbegu mbili katika kila shimo na kupitizia drip irrigation.

Hili hufanyika kuanzia kila mwanzo wa tuta hadi mwisho wa matuta yaliyopangika vizuri ndani ya kitalu.

Anasema msimu wa kupanda nyanya huchukua miezi mitatu kukua.Kwa siku humwagilia maji mara mbili.

Otieno huvuna matunda ya nyanya kwa miezi sita mfululizo kabla ya mimea kukauka na akapanda tena upya mbegu zingine.

Wateja wake wengi ni kutoka mjini Nakuru,ambapo yeye huuza kilo moja ya nyanya kati ya 60-80.

Kila wiki hufikisha mazao yake katika maduka ya kijumla mjini Nakuru mara mbili yaani Nakumatt,Gilanis na Woollmatt.

Mathalan duka la Gilanis huchukua kilo 400 kila wiki ambazo humpatia Sh32,000 kwa wiki .

Ushauri wake kwa vijana ni wajifundishe nyenzo mbalimbali za kujiajiri kabla ya kuajiriwa..

You can share this post!

AKILIMALI: Mashine ya kisasa inayokata nyasi kwa kasi

BI TAIFA MACHI 10, 2019

adminleo