Michezo

NIPO KWA KAZI HII: Magoli ya CR7 yanusuru Juventus

March 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

TURIN, Italia

KABLA ya Juventus kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Atletico Madrid, staa Cristiano Ronaldo aliripotiwa kuwaambia marafiki na jamaa zake kwamba yuko katika kiwango kizuri cha kufunga mabao matatu.

Ndoto hiyo ilitimia Jumatano usiku alipopachika wavuni mabao matatu yaliyoiwezesha Juventus kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya.

Baada ya kushindwa 2-0 kwenye mkondo wa kwanza nchini Uhispania, Juventus walihitaji kufunga mabao ya kutosha ugani mwao Allianz Stadium mjini hapa ili kutinga hatua ya robo-fainali.

Baada ya kufunga mabao mawili mapema, Juventus walipewa mkwaju wa penalti ambao raia huyo wa Ureno aliyeonyesha umahiri mkubwa usiku huo alifunga kwa kishindo dhidi ya timu ambayo haijawahi kushindwa katika mechi tano zilizopita.

Fowadi Cristiano Ronaldo wa Juventus asherekekea baada ya kufunga mabao yote matatu kwenye kabiliano kali la Juve dhidi ya Atletico Madrid ambapo wenyeji walishinda 3-0 Machi 12, 2019, mjini Turin. Picha/ AFP

Iwapo, klabu hiyo ya Serie A itatwaa ubingwa wa ligi hiyo, hii itakuwa mara ya nne mfululizo kwa staa huyo kubeba taji hilo.

Kulikuwa na hofu huenda Juventus wakaondolewa katika hatua ya muondoano baada ya kichapo cha 2-0 katika awamu ya kwanza ya mechi hiyo, hali ambayo ingemfanya Ronaldo kushindwa kufika angalu nusu-fainali kwa mara ya kwanza tangu 2010, na mara ya pili katika misimu 12.

Ronaldo alifunga bao la kwanza dakika ya 27 baada ya kuruka juu kuliko mlinzi wa Atletico Junafran na kuipa timu yake matumaini ya kubadilisha matokeo ya mkondo wa kwanza.

Afunga bao la pili

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34 alifunga bao la pili dakika nne baada ya muda wa mapumziko.

Ronaldo aliyejiunga na Juventus kwa kitita cha Sh11 bilioni msimu uliopita akitokea Real Madrid alisema jukumu lake ni kuisaidia Juventus kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa.

“Hii ndio sababu iliyoifanya Juventus kunileta hapa,” alisema nyota huyo ambaye kufikia sasa amefunga mabao 18 katika 14 za hatua ya muondoano kwenye mechi hizi za Ulaya.

 “Ari hii inahitajika ili kushinda ubingwa wa michuano hii. Tulicheza vizuri kwa makini. Wapinzani wetu walikuwa wakali, lakini pia sisi tulikuwa tumejiandaa vyema. Tunasubiri kitakachotokea kwenye ratiba itakayofuata.”

Baada ya uchezaji wake wa hali ya juu, aliyekuwa nahodha wa Manchester United, Rio Ferdinand alisema Ronaldo atabakia kuwa ‘mbabe’ wa soka kutokana na kile alichoifanyia Juventus Jumatano usiku, mbali na timu nyingine alizochezea hapo awali.

“Katika ligi ya mabingwa, Ronaldo amevunja rekodi zote. Na sasa ameshinda Atletico Madrid timu inayosifika kuwa kuwa na ulinzi mkali kwa sasa,” alisema Ferdinand.

Kocha wa Atletico, Diego Simeone alisema kukosekana kwa straika Diego Costa kutokana na marufuku ya kadi nyekundu kulivuruga mipango yake.

Alvaro Morata aliyepewa nafasi hiyo kusaidiana na Antoine Griezmann alishindwa kuokoa timu yake ambayo iliingia uwanjani ikijivunia ushindi wa 2-0.

Wakati Griezmann akipewa asilimia 6.0 kwa 10, Ronaldo alipata asilimia 9.8, huku kipa Jan Oblak akipata akipata asilimia 5.4 pekee.