Habari Mseto

Turkana, Baringo na Pokot zalia njaa

March 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BARNABAS BII

MAELFU ya familia zinazokumbwa na baa la njaa katika sehemu za Kaskazini mwa Bonde la Ufa zinahitaji usaidizi wa dharura wa chakula na huduma za afya.

Familia hizo, katika kaunti kame za Turkana, Pokot Magharibi na Baringo, zinakumbwa na uhaba wa chakula, maji na lishe ya mifugo wao kwa kipindi cha miezi miwili sasa.

Tayari, Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Kiangazi (NDMA) imetoa tahadhari kuhusu athari za kiangazi hicho.

Mamlaka ilisema kwamba uhaba wa chakula umekuwa ukienea tangu Januari, kwani sehemu nyingi hazijapokea mvua ya kutosha tangu wakati huo.

Wengi miongoni mwa walioathiriwa wamehamia nchini Uganda kutafuta chakula na malisho kwa mifugo wao, hasa wanaoishi katika Kaunti Ndogo ya Pokot Kaskazini.

Jana, viongozi kutoka kaunti hizo waliomba serikali na mashirika ya kutetetea haki za binadamu kuharakisha usambazaji wa misaada na utoaji wa huduma za afya.

Katika Kaunti ya Turkana, familia zaidi ya 300,000 zinakumbwa na uhaba wa chakula, baada ya mimea yao kukauka.

“Serikali inapaswa kutangaza hali hii kama janga la wa kitaifa na kuanza usambazaji wa chakula cha msaada,” akasema Mbunge wa Kike wa Kaunti ya Turkana, Bi Joyce Emanikor.