• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:50 AM
Sikumfuta kazi Matiang’i, asema Magoha

Sikumfuta kazi Matiang’i, asema Magoha

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi Profesa George Magoha amekanusha madai kwamba ni yeye aliyeidhinisha kufutwa kazi kwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alipokuwa mhadhiri katika chuo hicho mnamo 2009.

Aidha, ameiambia kamati ya bunge kuhusu uteuzi, iliyompiga msasa kubaini ufaafu wake kushikilia wadhifa wa Waziri wa Elimu, kwamba Dkt Matiang’i ndiye alipendekeza uteuzi wake kuwa mwenyekiti wa Baraza la Mitihani (KNEC) mnamo 2015.

Akijibu maswali ya wabunge, Magoha amesema Dkt Matiang’i alifutwa kazi na wadogo wake ambao aliwapa uhuru wa kuendesha idara zao.

“Mheshimiwa Spika japo sipendi kujadili watu, lakini nakubali kwamba nina uhusiano wa karibu na Dkt Matiang’i kwani nilikuwa bosi wake katika chuo kikuu kisha akawa bosi wangu nilipohudumu kama mwenyekiti wa Knec. Hata hivyo, nitajibu kwa kusema kuwa sikuidhinisha kufutwa kwake kwani shughuli hiyo iliendeshwa na wadogo wangu,” akasema Prof Magoha.

Profesa Magoha alisema hayo akijibu swali kutoka kwa Mbunge wa Kikuyu, Kimani Ichung’wa ambaye alitaka kujua kwa nini aliorodhesha Dkt Matiang’i shahidi (referee) wake katika wasifukazi aliyowasilisha bungeni ilhali waziri huyo “alifutwa kazi chini ya usimamizi wako.”

“Vilevile, nataka aeleze jinsi watafanya watakavyofanya kazi ikiwa kamati hii itaidhinisha uteuzi wake kwani sasa Dkt Matiang’i atakuwa bosi wake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri kuhusu Utekelezaji wa Miradi ya Serikali,” akauliza Ichung’wa.

Ajikanganya

Hata hivyo Profesa Magaha alionekana kujikanganya kwa sababu awali aliiambia kamati hiyo inayoongozwa na Spika Justin Muturi kuwa mtindo wake wa utendekazi ni wa kuwapa wadogo wake uhuru wa kufanyakazi lakini “kwa kufuatilia kwa karibu kuhakikisha mambo hayaendi kombo.”

Lakini ya kuteuliwa kuwa Waziri mnamo 2013, Dkt Matiang’I alikuwa mhadhiri katika Idara ya Fasihi ya Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Lakini duru zinasema alipigwa kalamu kupitia barua iliyoandikia na aliyekuwa Msaidizi wa Naibu Chansela Profesa Peter Mbiti kwa kwa kukwepa majukumu yake na kujihusisha na mipango ya Shirika la Center for International Development (CID) iliyosimamiwa na Chuo Kikuu cha New York.

Alhamisi Profesa Magoha aliahidi kulainisha sekta ya elimu endapo wabunge wataidhinisha uteuzi wake huku akitaja rekodi yake ya utendakazi katika chuo kikuu cha Nairobi na Knec.

“Nataka kutoa hakikisho kwa kamati hii kwamba nitachapa kazi bila mapendeleo kwa misingi ya kisiasa, kimaeneo au kikabila. Lakini nitakuwa nikishauriana na wadau wote kuanzia Rais, ninyi kama wabunge na maafisa wa wizara, kabla ya kufanya maamuzi,” akasema.

Profesa Magoha amesema anaunga mkono mtaala mpya wa masomo kwa sababu malengo yake yanalandana na hitaji la kuwapa watoto ujuzi ambao utawafaa kujisaidia maishani.

“Lakini ningeomba kamati hii kuhakikisha kuwa pesa za kufanikisha utekelezaji wa mfumo huo wa elimu unatolewa kwa wakati,” akasema huku akiongea kuwa tayari mtaala huo unatekelezwa katika mataifa ya Rwanda na Sudan Kusini.

You can share this post!

Mpasuko zaidi Jubilee wabunge wakikabana koo

Thamani ya Prof Magoha ni Sh250 milioni

adminleo