• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Murkomen amtaka Uhuru ampige kalamu Kinoti

Murkomen amtaka Uhuru ampige kalamu Kinoti

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kumfuta kazi mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti.

Bw Murkomen ambaye ni seneta wa Elgeyo Marakwet anataka Bw Kinoti apigwe kalamu kwa kile anachataja kama hatua yake ya kuingiza mapendeleo katika uchunguzi wa sakata za ufisadi unaoendeshwa na afisi yake kwa sasa.

Alimsuta afisa huyo kwa kutoa habari kuhusu uchunguzi wake kwa vyombo vya habari kabla ya wahusika kuhojiwa.

“Vyombo vya habari vilituambia kwamba Rotich angeulizwa maswali 300 hata kabla ya waziri huyo kuagizwa kufika katika makao makuu ya DCI. Nilidhani ilikuwa ni propaganda kabla nilipofahamishwa kwamba kweli aliulizwa maswali 300,” Bw Murkomen akasema katika halfla ya kuchanga pesa za kuisaidia Shule ya Upili ya Wasichana ya Koiwalelacha iliyoko eneo bunge la Belgut, kaunti ya Kericho.

Waziri wa Fedha Henry Rotich alihojiwa na maafisa wa DCI siku tatu mfululizo kuhusu sakata ya Sh21 bilioni zilizolipwa na serikali kwa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Pesa hizo zililipwa kwa kampuni mbalimbali zilizohusishwa na miradi licha ya kwanza kazi haijaanza na wakazi wa eneo hilo hawajalipwa ridhaa kwa ardhi ambako mabwawa hayo yatajengwa.

“Hatuwezi kupambana na ufisadi kwa njia hii. Vita hivi sharti viendeshwe bila mapendeleo. Tunamtaka DCI kuendesha kazi hii kitaalamu,” Bw Murkomen akasema.

Vile vile alimwonya Bw Kinoti dhidi ya kutumiwa kuwaangusha wanasiasa fulani.

“Ningependa kumwambia DCI kufuata sheria na aruhusu washukiwa wachunguzwe kwa misingi ya ushahidi sio chuki za kisiasa,” Bw Murkomen akaeleza.

Alidai kuwa wanasiasa fulani wamekuwa wakimtembelea Bw Kinoti kupambana namna ya kuwekelea makosa mahasidi wao wa kisiasa.

“Vile vile, nina haari kwa Bw Kinoti amekuwa akitaka nichunguzwe kwa madai ya ufisadi lakini ameshindwa kunihusisha na sakata yoyote,” akasema.

Bw Murkomen alikuwa ameandamana na seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot, Mbunge wa Belgut Nelson Koech, Hillary Koskei (Kipkelion Magharibi). Wengine walikuwa wabunge; Sylvanus Maritim (Ainamoi), Joseph Limo (Kipkelion Mashariki), Dominic Koskei (Sotik) na Kipsengeret Koros (Soin/Sigowet).

Viongozi hao pia walitaka afisi ya DCI itenganishwe na Huduma ya Kitaifa ya Polisi ili iwe huru.

Kimsingi DCI hufanya kazi chini ya uelekezi, amri na usimamizi wa Inspekta Jenerali wa Polisi.

“Kuondolewa kwa afisi ya DCI kutoka kwa idara ya polisi kutaikinga dhidi ya kutumiwa kwa sababu za kisiasa,” akasema Bw Cheruiyot.

“Tunataka afisi ya DCI kuwa huru ili mshikilizi asishawishiwe na wanasiasa,” akaongeza.

Naye Bw Koskei alisema DCI anafaa kuteuliwa kwa njia ya ushindani sio moja kwa moja ilivyo sasa ambapo Kinoti anaonyesha uaminifu kwa wanasiasa fulani ambao lengo lao ni kuwajumu wapinzani wao.

Kando na Bw Rotich, mawaziri Eugene Wamalwa (Ugatuzi) na Mwangi Kiunjuri (Kilimo) pia wamehojiwa kuhusiana na sakata hiyo.

You can share this post!

TAHARIRI: Agizo la Rais kuhusu ufadhili litekelezwe

Agora wasanii wenye azma ya kufikia upeo wa Wasafi Classic...

adminleo