• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:55 PM
Waziri alalamikia ongezeko la baa na ulaji muguka

Waziri alalamikia ongezeko la baa na ulaji muguka

Na GEORGE MUNENE

WAZIRI wa Afya Sicily Kariuki amelalamikia ongezeko la idadi ya baa katika Kaunti ya Embu na kuitaka serikali ya kaunti hiyo kuacha kutoa leseni za biashara hiyo.

Bi Kariuki alisema kuwa baa zimeanzishwa katika vijiji na karibu na shule kila kona ya kaunti hiyo.

“Katika kijiji ambako ninatoka, kuna baa kumi na hali hii sasa inaanza kuhofisha,” Bi Kariuki alieleza wakazi Ijumaa, alipokuwa mjini Siakago, eneo la Mbeere wakati wa matibabu ya bure yaliyoandaliwa na Muungano wa Wataalamu wa Embu.

Takriban wakazi 1,000 ambao walitoka maeneo tofauti ya kaunti hiyo walitibiwa magonjwa tofauti na madaktari wa kujitolea.

Waziri huyo alisisitiza kuwa kuna haja ya kupunguza idadi ya baa, ambapo wanafunzi kutoka shule mbali mbali huenda kunywa pombe.

“Kufunguliwa kwa baa karibu na vituo vya elimu na vijijini ni kuhatarisha wanafunzi kwa kuwafanya waanze kutumia pombe. Shughuli ya kaunti kutoa leseni inafaa kudhibitiwa na kufuatiliwa vyema,” alisema.

Alimtaka Mshirikishi kamishna wa kaunti hiyo Abdulahi Galgalo na maafisa wa polisi kuhakikisha kuwa baadhi ya baa ambazo ziko maeneo aliyolalamikia zimefungwa, akisema Embu inageuka kuwa eneo la walevi. Aidha, waziri alilaumu biashara ya muguka kama tatizo kwa elimu eneo hilo akisema watoto hawafai kushirikishwa.

“Biashara hii inafaa kuachiwa watu wazima pekee kwani inaharibu vizazi vidogo,” waziri huyo aliongeza.

Mwenyekiti wa muungano huo Ibrahim Mwathane aidha alikubaliana na matamshi ya Bi Kariuki, akisema kwahitajika juhudi nyingi ili kuhakikisha kuwa tatizo la dawa za kulevya eneo hilo miongoni mwa watoto linakabiliwa haraka.

You can share this post!

AP aliyedaiwa kuua mwalimu anaswa akivuka mpaka

Handisheki ilichangia kutimuliwa kwangu, Echesa sasa alia

adminleo