Handisheki ilichangia kutimuliwa kwangu, Echesa sasa alia
Na IBRAHIM ORUKO
ALIYEKUWA waziri wa Michezo Rashid Echesa, amelaumu ‘handisheki’ kati ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga kwa kufanya afutwe kazi.
Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Jumapili, Bw Echesa alimlaumu Bw Odinga kwa kuvuruga mambo katika serikali na kumchochea Rais dhidi ya maafisa wake.
Bw Echesa, ambaye alihusishwa na sakata nyingi siku zake za mwisho kama waziri, alisema ingawa Rais hakumpa sababu za kumfuta kazi, anaamini kulichangiwa na siasa.
“Sijawahi kupewa sababu halisi za kufutwa kwangu na ikulu, ila ni amri tu aliyotoa Rais. Ingekuwa vyema ikiwa ningeambiwa sababu za kufutwa ili nikipata fursa nyingine ya kuhudumu katika serikali, nisirudie makosa hayo,” alisema Bw Echesa.
Alisema tangu kiongozi huyo wa ODM alipoafikiana na Rais Kenyatta mwaka 2018, ndipo mambo yalipoanza kumwendea mrama.
“Kabla ya ‘handisheki’ mambo yalikuwa shwari serikalini. Lakini kupenya kwake serikalini kupitia muafaka kuliharibu mambo kabisa. Anaonekana kama aliyemfanyia kitu Rais ambaye tangu wakati huo amebadilika.
“Tangu wakati huo Rais aligeuka na kuanza kuwa na hasira, hacheki kwa urahisi, na kila wakati anaonekana tayari kugombana. Namlaumu Bw Odinga kwa hili. Alimaliza furaha yetu katika serikali,” alisema Bw Echesa.
Alisema tangu siku ya kwanza ya handisheki, hakujakuwa na amani katika serikali na miongoni mwa mawaziri.
“Mawaziri hawana amani, wote wamekaa roho mikononi, wakihofia kuhusu kukemewa mbele ya umma ama kufutwa kazi wakati wowote. Kila kitu kilibadilishwa na ‘handisheki’,” alisema Echesa.
Akieleza kuhusu uhusiano wake na Rais siku zake za uwaziri, Bw Echesa alisema kabla ya handisheki walikuwa na uhusiano mwema, lakini mambo yaliharibika baadaye.
Bw Echesa alilaumiwa kwa kujihusisha na siasa za uchaguzi wa 2022 kwa kumuunga Naibu Rais William Ruto anayetarajiwa kushindana na Bw Odinga.
Bw Echesa, hata hivyo, alipinga madai ya kuhusishwa na sakata kadhaa siku za majuzi (kabla ya kufutwa kazi) ambapo alikuwa amedaiwa kuwa alikuwa na uhusiano na mmoja wa washukiwa walioshtakiwa kwa kumlaghai mfanyabiashara mamilioni ya pesa, kwa kuiga sauti ya Rais Kenyatta.
Vilevile, waziri huyo wa zamani alipinga madai kuwa anamiliki nyumba ambamo watu walikamatwa, wakidaiwa kuwa na pesa feki Sh32 bilioni eneo la Ruiru.
Alisema madai hayo yamekuwa yakisukumwa na mahasimu wake wa kisiasa ambao wanalenga kumchafulia jina, akishangaa kwa nini polisi hawajamchukulia hatua ikiwa ni kweli.
Lakini alisema anashukuru kwa muda aliohudumu kama waziri, akisema lilikuwa azimio kuu katika maisha yake.
“Sijui kama nitawahi kufanya kazi ya uwaziri tena lakini nimeachwa na kumbukumbu ambazo nitawahadithia wajukuu wangu,” alisema.