Habari MsetoSiasa

Joho na Kingi sasa waombwa kuungana kabla ya 2022

March 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMUEL BAYA

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi, Amason Kingi wamehimizwa wajadiliane na kuamua nani kati yao atagombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Wawili hao ambao wanahudumu kipindi cha mwisho, wametangaza kuwa watagombea urais kwenye Uchaguzi wa Mkuu wa 2022.

Japo Gavana Joho anasisitiza atakuwa debeni kwenye kura ya Urais ifikapo 2022, Bw Kingi pamoja na wafuasi wake wanasisitiza kuwa sharti kuwe na mashauriano ya eneo la Pwani kuamua atakayepeperusha bendera yao.

Akizungumza katika hafla moja eneo la Rabai mnamo Ijumaa, Bw Joho alisema kuwa eneo hilo limeamua sharti litoe mwaniaji urais, akisema wakazi wa Pwani pia wanahitaji kuwa na uwakilisi katika siasa za kitaifa.

“Sharti tujiamini kama wanabondia hata ikiwa tunaenda uwanjani kukabiliana na mtu mkubwa, huenda hana uwezo wa kutushinda,” Gavana Joho alisema.

“Kwa uwezo wa Mungu, wakati huu tutakuwa katika siasa za kitaifa. Hata kama hatutafurahisha, tutakuwa debeni 2022,” alisema.

Gavana huyo alisema viongozi wa eneo hilo waliamua kuunga mkono Muafaka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, ili kuimarisha vita dhidi ya ufisadi.

“Tuliamua kuwaunga mkono Rais Kenyatta na Bw Odinga katika vita dhidi ya ufisadi ili tukiingia uongozini katika serikali inayofuata, tuwe tumemaliza uovu huo kabisa,” akasema.

Mbunge wa Mathare Anthony Oluoch ambaye alikuwa katika hafla hiyo alisema kuwa endapo Bw Odinga ataamua kustaafu, Bw Joho yuko katika nafasi nzuri ya kuchukua hatamu.

“Raila akitwambia kuwa anastaafu siasa za kitaifa, mtu wa pekee tunayejua atampendekeza ni Joho,” akasema Bw Oluoch. Lakini naibu wa gavana Kaunti ya Kilifi, Gideon Saburi ambaye alikuwa katika hafla hiyo kumwakilisha Bw Kingi, alisema kuwa sharti mkubwa wake aketi na Bw Joho na kuelewana atakayepeperusha bendera ya urais kutoka eneo hilo.

“Tulikuwa na mkutano mkubwa wa viongozi wa pwani ambao ulihudhuriwa na magavana wote wawili. Walituahidi kuwa kabla ya wakati huo, watakuwa wamefanya uamuzi na kutuelekeza. Tunawapenda wote na tutatii kile watakachotuambia,” Bw Saburi akasema.

Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire naye, ambaye ni naibu mwenyekiti wa ODM kaunti ya Kilifi alisema kuna haja kwa viongozi hao wawili kuzungumza na kuwa na sauti moja.