• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
JAMVI: Hofu ‘Tanga Tanga’ wanampumbaza Ruto kuhusu 2022

JAMVI: Hofu ‘Tanga Tanga’ wanampumbaza Ruto kuhusu 2022

Na WANDERI KAMAU

KIMYA cha waandani wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Kati kuhusu vita vinavyoendelea dhidi ya ufisadi kimeibua wasiwasi kwamba huenda wanamhadaa kisiasa kuhusu ahadi ya kumuunga mkono 2022.

Kundi la ‘Tanga Tanga’ ambalo limekuwa likimtetea vikali Bw Ruto limebaki kimya, licha ya waandani wake katika eneo la Bonde la Ufa kujitokeza vikali kumtetea kuhusu tuhuma za kuhusishwa katika ufisadi.

Miongoni mwa viongozi ambao wamejitokeza wazi kumtetea Dkt Ruto ni mbunge Oscar Sudi (Kapseret), maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Aaron Cheruiyot (Kericho) kati ya wengine.

Kundi la ‘Tanga Tanga’ linajumuisha wabunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Ndindi Nyoro (Kiharu), Rigathi Gachagua (Mathira), magavana Ferdinard Waititu (Kiambu), Mwangi wa Iria (Murang’a) kati ya wengine.

Kulingana na wachanganuzi, dhana ya hadaa hiyo iliibuliwa majuzi na Gavana Waititu, alipodai kwamba vita dhidi ya ufisadi vinahatarisha usalama wa jamii ya Agikuyu inayoishi katika eneo la Bonde la Ufa.

“Tunafurahi kwamba Rais Uhuru Kenyatta amejiotolea kuimarisha vita dhidi ya ufisadi. Hata hivyo, lazima juhudi hizo ziendeshwe kwa hali ambayo haitahatarisha watu wetu (Agikuyu) wanaoishi katika Bonde la Ufa,” akasema Bw Waititu.

Kwa hayo, wachanganuzi wanasema ni dhahiri kuwa kimya cha kundi hilo na matamshi ya Bw Waititu kinaashiria kwamba lengo lao kuu ni kuilinda jamii hiyo, ila si nia ya kumuunga mkono Bw Ruto.

“Ni wazi kwamba Dkt Ruto ametajwa sana kwenye vita dhidi ya ufisadi. Tungetarajia kuwaoa viongozi hawa wakijitokeza wazi kumtetea. Kimya chao bila shaka ni ishara inayoonyesha kwamba kunaa hadaa fiche iliyopo,” asema wakili Ndegwa Njiru.

Kulingana na mchanganuzi huyo, ingekuwa sawa ikiwa viongozi hao wangejitokeza kumtetea Dkt Ruto sawa na vile ambavyo wamekuwa wakimhakikishia kumuunga mkono mnamo 2022.

“Mbona wamekimya? Ni hali inayoonyesha hadaa kubwa kwa viongozi hao. Ikiwa ni kweli wanajali mustakabali wake, wangeonekana wakimtetea sawa na wenzao katika Bonde la Ufa,” asema wakili huyo.

Kundi hilo limekuwa likimhakikishia Ruto kwamba eneo la Mlima Kenya litamuunga mkono kuwania urais mnamo 2022.

Wachanganuzi wanasema kwamba isingalikuwa kimya cha waandani hao, Dkt Ruto hangefikia kiwango cha kujitokeza kudai kwamba Idara ya Upelelezi (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) wanawalenga baadhi ya watu kwenye vita dhidi ya ufisadi.

“Kauli ya Dkt Ruto Jumapili iliyopita katika eneo la Pwani kwamba kuna baadhi ya watu wanaolengwa ni ishara ya wazi kwamba anahisi kuwa viongozi aliowekeza kumtetea hawafanyi hivyo. Hili ni jambo ambalo hangefanya ikiwa waandani wake katika Mlima Kenya wangekuwa wakimtetea,” asema Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa.

Hata hivyo, Bw Muga anasema kwamba huenda kuna sababu kadhaa ambazo zimewafanya wabunge hao kunyamaza, baadhi zikiwa kutoonekana kutopinga juhudi za Rais Uhuru Kenyatta kupigana na ufisadi.

Asema kwamba ikizingatiwa wengi bado wanahudumu katika vipindi vya kwanza, hawangetaka kuukasirisha umma, kwani hilo linahatarisha nafasi ya kurejeshwa tena Bungeni mnamo 2022.

“Rais Kenyatta bado ana ushawishi mkubwa wa kisiasa katika eneo la Mlima Kenya. Hili linamaanisha kwamba kuna uwezekano mkubwa wakazi kutiii na kuzingatia mwelekeo wa kisiasa atakaowaomba kuzingatia. Hilo bila shaka litaathiri pakubwa hatima yao ya kisiasa,” asema Bw Muga.

Kando na hayo, Bw Muga anasema kuwa kando na kuhofia hatima yao kisiasa, baadhi yao wanaonekana kutii agizo la Rais Kenyatta kutoendeleza kampeni za 2022.

Jamii ya Agikuyu imekuwa mwathiriwa mkuu wa vita vya kikabila katika eneo la Bonde la Ufa, hali iliyochangia Rais Kenyatta na Dkt Ruto kubuni ushirikiano wa kisiasa mnamo 2012 baada yao kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutokana na vita vilivyotokea baada ya uchaguzi tata wa 2007.

Wachanganuzi wanasema mwelekeo wa siasa za 2022 ni sawa na 2007, ila mara hii viongozi wa Kati wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba hakuna mzozo wowote unaoibuka kati ya jamii za Agikuyu na Wakalenjin.

“Kwa kimya hicho, ni dhahiri kwamba kuna uwezekano kwamba kundi la Tanga Tanga ni njia tu ya kumpofusha Ruto kuhusu 2022, kwamba atapokea uungwaji mkono kutoka Mlima Kenya, ila iwe ni hadaa tamu,” asema Kiprotich Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Mnamo Januari, Rais Kenyatta aliwaagiza wabunge wote wa Jubilee kuangazia masuala ya maendeleo, badala ya kuendeleza kampeni.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge walimwasi, ila wachanganuzi wanaeleza kuwa huenda kimya chao kikaashiria madhara ya kisiasa ambayo huenda yakawakumba.

“Wabunge hao hawataki kuonekana kuwa kikwazo hata kidogo kwenye vita dhidi ya ufisadi. Huenda ikawa njia moja ya kiishara kueleza kwamba wanamuunga mkono Rais, ijapokuwa wanaangazia mustakabali wao kisiasa,” akasema.

You can share this post!

JAMVI: Huenda shinikizo za wandani wa Ruto kwa Uhuru...

Ulinzi na Sofapaka zatupwa nje ya SportPesa Shield

adminleo