• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Si hatia kuendesha gari ukiwa mlevi, jaji asema

Si hatia kuendesha gari ukiwa mlevi, jaji asema

Na JOSEPH WANGUI

MAHAKAMA Kuu ya Nyeri iliamua Jumatatu kuwa uendeshaji gari ukiwa mlevi si hatia mradi dereva aweze kulithibiti gari.

Uamuzi huu wa Jaji Teresiah Matheka, umeonekana kutatiza kampeini za kuhamasisha madereva wasiendeshe magari wakiwa walevi.

“Kuwa na pombe mwilini sio hatia. Makosa ni kushindwa kulithibiti gari unapoendesha.Haya ndiyo maneno katika Kifungu cha Shera 44(1) za Trafiki,” alisema Jaji Matheka.

Jaji Matheka alifafanua haya alipotoa uamuzi katika rufaa iliyowasilishwa na dereva wa matatu, Bw George Wambugu Thumbi.

Bw Thumbi alikuwa amepinga adhabu ya faini ya Sh100,000 aliyotozwa na Hakimu Mkuu wa Nyeri, Bi Wendy Kagendo mnamo Januari 2, 2018.

Endapo alishindwa kuilipa mshtakiwa aliagizwa atumikie kifungo cha mwaka mmoja gerezani kwa kupatikana akiendesha gari la kubeba abiria akiwa mlevi.

Hakimu pia alikuwa amefutilia mbali leseni ya Bw Thumbi kwa kipindi cha miezi sita.

Jaji Matheka, aliulaumu upande wa mashtaka na hakimu kwa kumfungulia mlalamishi mashtaka mawili yanayolingana kinyume cha vifungu viwili vya sheria za trafiki.

Jaji huyo alisema kila mojawapo ya sheria hizo inajisimamia kivyake na makosa yalifanywa kumshtaki Bw Thumbi kwa mujibu wa sheria zote mbili.

“Dereva huyu alidhulumiwa kwa kushtakiwa kwa sheria zote mbili ilhali upande wa mashtaka ulikuwa umeahidi kuthibitisha kesi mbili katika cheti kimoja,” alisema Jaji Matheka.

You can share this post!

Maraga ahimiza vituo vya polisi vikumbatie mfumo wa...

Mfungwa aliyetoroka ajirejesha gerezani

adminleo