Habari MsetoSiasa

Kero baa la njaa kuwafaidi wanasiasa

March 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

SERIKALI Jumatatu ilitoa Sh2 bilioni za kuwalisha Wakenya wanaokabiliwa na njaa maeneo mbalimbali ya nchi.

Kiasi hicho ni cha chini ikilinganishwa na Sh6 bilioni ambazo Wizara ya Ugatuzi ilikuwa imeomba kuwezesha kutolewa kwa chakula cha msaada kwa wakazi hasa katika kaunti za Turkana, Baringo, Samburu, Marsabit, Mandera, Wajir na Garissa.

Zingine ni Isiolo, Kilifi, Tana River, Pokot Magharibi, Makueni, Kajiado na Kwale.Akitangaza mpango huo, Naibu Rais William Ruto aliahidi kuchukuliwa kwa kila hatua kuhakikisha wote wanaokabiliwa na njaa wameshughulikiwa.

Alisema hayo baada ya kukutana na mawaziri Henry Rotich (Fedha), Mwangi Kiunjuri (Kilimo), Eugene Wamalwa (Ugatuzi) na Simon Chelugui (Maji).

Lakini huku maelfu wakiumia njaa na kuwa kwenye hatari ya kufa, kutolewa kwa pesa hizo ni furaha kwa makundi na watu binafsi ambao watahusika katika shughuli ya hiyo ya utoaji wa chakula cha msaada.

Makundi hayo yanajumuisha wanasiasa, machifu na manaibu wao, wafanyabiashara, wasafirishaji na mashirika yasiyo ya serikali (NGOs).

Katika miaka ya awali, wanasiasa wamekuwa wakichukua fursa ya ugawaji wa chakula cha misaada kujitafutia umaarufu na pia kuingilia shughuli hii, ili kuhakikisha wanaonufaika zaidi ni wafuasi wao.

Hali ya njaa pia huwa fursa kubwa kwa wafanyabiashara, ambao hupata soko la nafaka, mafuta na vyakula vingine vya misaada, ambavyo hununuliwa kwa ajili ya kuwalisha waathiriwa.

Mtandao huo pia huwashirikisha wasafirishaji, ambao mara nyingi hupewa kandarasi za kusafirisha chakula kinachotolewa.

Wengi wa wasafirishaji hao huwa washirika wa karibu wa kibiashara na kisiasa wa maafisa wanaohusika katika shughuli za usambazaji.Mtandao huo pia unawashirikisha baadhi ya maafisa wa utawala, ambao hutumia nguvu zao kuamua wananchi ambao watafikiwa na chakula hicho.

Baadhi wamekuwa wakilaumiwa kwa kuficha chakula wanachopewa kuwasambazia wananchi na baadaye kukiuza.

Kundi jingine ambalo limekuwa likitumia njaa kujitajirisha ni wanunuzi mifugo, ambapo huwanunua kwa bei ya chini kwani wengi huwa wamedhoofika kwa kukosa malisho.

Mashirika yasiyo ya kiserikali pia hunufaika pakubwa kwa kutumia suala la njaa kuomba ufadhili ng’ambo na hata hapa nchini, huku kiasi kikubwa wanachopata kikikosa kufikia wanaolengwa.

Wakati wa kikao cha jana, Serikali ilikanusha kwamba watu kadhaa wamefariki kutokana na makali ya njaa nchini, hasa katika kaunti za Baringo na Turkana.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Kiangazi (NDMA) James Oduor, alisema matokeo ya uchunguzi wao ni kwamba vifo hivyo vilitokana na maradhi ya kawaida.