• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
Wakenya wamtafuna Ruto kudai hakuna mtu ameangamia kwa njaa nchini

Wakenya wamtafuna Ruto kudai hakuna mtu ameangamia kwa njaa nchini

Na PETER MBURU

WAKENYA kwenye mitandao ya kijamii wamemshambulia Naibu Rais William Ruto kufuatia matamshi yake mara mbili sasa kuwa hakuna Mkenya yeyote amekufa kutokana na baa la njaa linaloendelea kukumba baadhi ya maeneo nchini, wakisema ameonyesha upuuzi.

“Hakuna mtu ameangamia kutokana na baa la njaa. Mnayosikia ni habari feki. Tunawahoji machifu wanaodai watu 11 wamefariki ili kuwachukulia hatua. Kwa sasa hatuna tatizo la baa la njaa nchini, tatizo lililopo ni usambazaji wa chakula. Hili ni suala nyeti ambalo halifai kuingizwa mzaha. Tutahakikisha hakuna Mkenya ataangamia kwa njaa,” Dkt Ruto alisema Jumatano jijini Mombasa.

Wakenya aidha wameshangaa sababu ya kutaka baadhi ya maafisa wa serikali kuadhibiwa baada ya kudokeza kuwa katika maeneo yao kuna watu waliokufa, wakionyesha kughadhabishwa na serikali.

Wakitoa hisia zao baada ya Dkt Ruto kusema kuwa bado taifa lina chakula cha kujitosheleza, Wakenya walimkashifu Naibu Rais wakisema wamejionea kwa macho matokeo ya kiangazi na njaa kupitia vyombo vya habari.

“Wacheni kuadhibu machifu, watu wanateseka na njaa hadi kufa, vyombo vya habari havitudanganyi,” akasema Kimani Chege, mtumizi wa Facebook.

Wakenya walisema kuwa machifu, ambao ndio wanafanya kazi karibu zaidi na wananchi ndio wanaelewa hali halisi na hivyo hawafai kuadhibiwa kwa kueleza shida zinazokumba jamii zao.

“Ni vibaya sana kuwa maafisa wa juu serikalini wanafanya hivi, wanataka kwenda kujionea wenyewe? Na ikiwa ni hivyo, kwani kazi ya machifu ni gani?” akasema Joseph Sifuna.

Wengi wa Wakenya waliona kuwa kiongozi huyo anapuuza ripoti za watu kufa kwa kuwa yeye mwenyewe hajaathirika, wakishangaa kuhusu uadilifu wake uongozini.

“Kama wewe umeshiba funika tumbo, Wakenya wanakufa wacha siasa duni,” akasema Wanjiru Wanjiru.

“Machifu ndio wako karibu zaidi na raia wa kawaida na hivyo wanajua idadi (ya watu ambao wameathirika),” naye Michael Samora akasema.

Wakenya wengi waliiona kuwa kawaida ya serikali kupinga kila kitu ambacho kinaionyesha kutotekeleza majukumu yake ipasavyo.

Wengine hata walitumia mbinu za kejeli kuonyesha kughadhabishwa kwao na Naibu Rais. “Rais wetu wa 2022 amezungumza, tafadhalini acheni kufa ama machifu na madiwani wetu watapoteza kazi,” akasema Judy Nyabera.

You can share this post!

Mizabibu inamhakikishia mkulima faida tele

Mvulana amuua mpenzi wa mamake

adminleo