• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
UTANI KANDO: Kane awarai wenzake kuzima tofauti baina yao kwa ajili ya taifa

UTANI KANDO: Kane awarai wenzake kuzima tofauti baina yao kwa ajili ya taifa

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MWANASOKA Harry Kane wa timu ya taifa ya Uingereza, amesisitiza kwamba uhasama miongoni mwa wachezaji wa klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hautaathiri kikosi cha kocha Gareth Southgate.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uingereza Harry Kane (kulia) akishauriana na kocha wake, Gareth Southgate wakati wa mechi mojawapo ya awali. Picha/ Maktaba

Mshambuliaji huyo wa kimataifa alisema hayo kufuatia upinzani mkali miongoni mwa klabu za Manchester City, Liverpool na Tottenham.

Manchester City watakutana na Liverpool kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) huku Tottenham wakicheza dhidi ya Manchester City katika mechi ya robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya.

Awali imekuwa vigumu kwa wachezaji wa timu ya taifa wanaochezea klabu za Liverool, Chelsea na Manchester United kutangazama wanapoitwa kambini kuchezea timu ya taifa.

Tofauti ya wachezaji wa timu ya Uingereza zimechangia kufanya vibaya kwa timu hiyo katika mashindano ya kimataifa, lakini Kane amesema chini ya Southgate, tofauti hizo hazitaonekana.

“Tunaelewa tofauti zilizokuwepo miaka iliyopita ambapo watu walikaa kwa misingi, lakini kikosi cha sasa hakina hiyo tabia. Tumekubaliana ni lazima tushirikiane kwa asilimia 100,” aliongeza staa huyo wa Tottenham Hotspur.

“Tofauti na ilivyokuwa zamani, kikosi hiki kina ushirikiano mkubwa. Tunataniana, tunacheka, lakini tunaelewa lengo letu kikosini. Hata wale wanaochezea Liverpool hawana tatizo na wenzao wa Manchester City. Lakini ni kawaida tunaporejea kwenye klabu zetu, ni kawaida watu kutumiana jumbe za kutisha. Tunapokuwa katika timu ya taifa, sisi ni marafiki wakubwa.”

“Ushirikiano wetu ndio uliotuwezesha kupiga hatua kubwa wakati wa fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi,” alisema nahodha huyo aliyeongoza wenzake kwenye mazoezi yaliyofanyika St Georges Park.

Mazoezi hayo kadhalika yalihudhuriwa na makinda, Declan Rice na Callum Hudson-Odoi ambao hii ni mara yao ya kwanza kuitwa kambini.

Jeraha dogo

Marcus Rashford alikuweko lakini hakushiriki mazoezini kutokana na jeraha dogo la kisigino, ambalo huenda likamkosesha gozi Ijumaa dhidi ya Jamhuri ya Czech katika pambano la Euro 2020, ugani Wembley.

Kuvuma kwao kwenye fainali za Kombe la Dunia ambako walitinga hatua ya nusu-fainali pamoja na kuimarika kwa klabu za Liverpool, Manchester City, Manchester United na Spurs katika michuano ya Klabu Bingwa kunaipa timu hiyo nafasi kubwa.

“Kuna wachezaji kadhaa wageni kikosini, na ni jukumu letu kuhakikisha wanajisikia vizuri na hali ilivyo. Lengo letu ni kuendelea kucheza vizuri huku tukilenga ushindi katika mechi zetu,” alisema Kane.

Baada ya kuitwa kikosini, Hudson-Odoi alisema: “Kwa hakika sijaamini baada ya kupokea habari hizo nzuri. Sio rahisi katika umri huu wangu kuitwa katika timu ya taifa. Nimefurahia na nitatia bidii zaidi katika maandalizi yangu.”

Kinda huyo aliyetambuliwa akiichezea timu ndogo ya Chelsea, kadhalika alivuma akiwa na timu ya taifa ya vijana.

You can share this post!

Ni afueni kwa Gor waratibu wa KPL wakipangua gozi

Huniambii chochote, Giggs amfokea Zlatan

adminleo