Kuna raha zaidi kuishi Somalia kuliko Kenya – Umoja wa Mataifa
Na PETER MBURU
KUISHI Somalia ni raha kushinda Kenya. Hii ni kulingana na utafiti ambao umefanywa na shirika la Umoja wa Mataifa (UN), kupitia kwa mradi wa kukagua maendeleo ya kisasa na ya kufaidi jamii, ambapo nchi 156 zimeorodheshwa.
Ripoti hiyo kwa jina ‘The World Happiness Report’ imeorodhesha Kenya kuwa nambari 121 kati ya mataifa yenye raha zaidi kuishi duniani, chini ya Somalia ambayo iko nambari 112.
Kulingana na utafiti huo kiwango cha raha nchini Somalia ni 4.668, wakati nchini Kenya ni 4.509.
Mataifa mengine ambayo yalishinda Kenya kwa raha ni barani Afrika Congo (Brazaville), Nigeria, Tunisia, Libya, Namibia na mengine mengi, lakini nchi yetu ikafanikiwa kushinda majirani wake Uganda (136) na Tanzania (153), na Sudan Kusini ambayo ilivuta mkia (156).
Mataifa yaliyoongoza kwa raha zaidi duniani ni Finland, Norway, Denmark, Sweden na Iceland. Kwa upande mwingine, yaliyovuta mkia ni Sudan Kusini, CAR, Afghanstan, Tanzania na Rwanda, kwa orodha hiyo kutoka mwisho.
Utafiti huo umelibaini taifa la Sudan Kusini kuwa baya zaidi kuishi duniani, kwani liliorodheshwa kuwa lenye raha ndogo zaidi, kwa alama 2.853.
Hii ni mara ya pili kwa UN kutoa ripoti kuhusu viwango vya raha katika mataifa ya dunia, na maslahi ya watu wa kutoka mataifa mengine ambao wanaishi katika nchi hizo. Utafiti mwingine ulifanywa mnamo 2012, ambapo Finland iliongoza.
Katika utafiti huu wa sasa, kati ya mataifa 10 ya mwisho, sita ni ya bara la Afrika, mengine yakiwa Yemen, Malawi, Syria, Botswana, Haiti na Zimbabwe.