Habari Mseto

Prof Magoha aidhinishwa na bunge kuwa Waziri wa Elimu

March 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wameidhinisha uteuzi wa Profesa George Magoha kuwa Waziri mpya wa Elimu kutoa nafasi kwa kuapishwa kwake wakati wowote kuanzia sasa.

Wabunge wa mirengo yote miwili Jumatano alasiri waliidhinisha ripoti ya Kamati ya Uteuzi iliyodhinisha uteuzi wake, wakimtaja kama mtu ambaye anahitimu zao kusimamia sekta ya elimu nchini.

Huku wakijadili ripoti ya kamati hiyo, wabunge hao walimiminia sifa Profesa Magoha kutokana na utendakazi wake wa kupigiwa mfano katika sekta ya umma.

Hadi wakati ambapo Rais Uhuru Kenyatta alimpendekeza kwa wadhifa huo, mnamo Machi 1, 2019, msomi huyo alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) ambako mageuzi aliyoanzisha yalipunguza visa vya wizi ya mitihani.

Vile vile, aliwahi kuhudumu kama Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi kuanzia 2005 hadi 2010. Na amekuwa mwenyekiti wa Bodi ya Madaktari na Wataalamu wa Meno Nchini (KMPDB)

Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa alielezea imani kuwa Profesa Magoha ndiye anayeweza kusuluhisha changamoto nyingi zinazosibu sekta ya elimu nchini.

“Nina uhakika kwamba atafanikiwa kwa sababu ana uhitimu, ujuzi, maarifa na uzoefu unaohitaji kwa wajibu huo. Hatutaki mawaziri wasio na tajriba yoyote kwa wizara muhimu kama hii ya elimu,” Dkt Wamalwa akasema.

Mbunge wa Seme James Nyikal alimtaja Profesa Magoha kama mtaalamu ambaye amedhihirisha kujitolea kwake katika utendakazi na kiwango cha juu cha uadilifu.

“Mara nyingi huchukuliwa kama mkakamavu kiasi cha ukakamavu huu kufasiriwa kumaanisha mtu mwenye sifa za mapuuza, lakini yeye hukubali makosa yake kwa urahisi mno,” akasema Dkt Nyikal.

Naye Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alimtaka Prof Magoha kama kiongozi ambaye husikiliza maoni na misimamo ya watu wengine.

“Ili watoto wetu waweze kupata elimu bora na kukua kama wanafunzi wanaomwogopa Mungu, Profesa Magoha sharti awe Waziri wa Elimu. Huu ndio uamuzi bora ambao umefanywa na Rais Kenyatta mwaka huu,” akasema Bw Owino.

Naye naibu kiongozi wa wengi Jimmy Angwenyi alimtaja Profesa Magoha kama mtu ambaye atataoa hisia zake waziwazi bila kuficha chochote. “Mtu kama huyu ndiye tunahitaji katika wizara ya elimu. Naamini kuwa atafanya elimu yetu kutambuliwa kote duniani,” akasem Bw Angwenyi ambaye ni Mbunge wa Kitutu Chache Kusini (Jubilee).

Wabunge wengine waliounga mkono uteuzi wa msomi huyo ni Kimani Ichungwa (Kikuyu, Jubilee), Dkt Robert Pukose (Endebess, Jubilee), Omboko Milemba (Emuhaya, ANC), Josephat Kabinga (Mwea, Jubilee), Ronald Tanui (Bomet ya Kati, Jubilee), Ezekiel Machogu (Nyaribari Masaba, Wiper) , kati ya wengine.

Sasa huenda Profesa Magoha akaapishwa Alhamisi na kuanza kazi mara moja. Anachukua nafasi ya Bi Amina Mohammed aliyehamishwa hadi Wizara ya Michezo kuchukua mahala pa Rashid Echesa aliyepigwa kalamu.