HabariSiasa

Akaunti za Twitter na Facebook za Uhuru zazimwa

March 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

AKAUNTI za mitandao ya kijamii za Rais Uhuru Kenyatta Ijumaa asubuhi zilizimwa, baada ya kudaiwa kuingiliwa na watu fulani bila idhini, saa chache baada ya ujumbe wa kuonya wafisadi kutumwa.

Mkuu wa wafanyakazi katika afisi ya Rais Nzioka Waita alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kama mbinu ya kurekebisha ambapo kulikuwa na makosa.

Bw Waita alisema wafanyakazi fulani wa afisi ya Rais ndio waliingilia akaunti zake za Twitter na Facebook, lakini akahakikisha kuwa hatua za kudhibiti hali zimechukuliwa.

“Kutokana na hali ya akaunti rasmi za mitandao ya kijamii ya Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta kuingiliwa bila idhini. Akaunti zote za Rais zimezimwa kwa muda ili hatua za kudhibiti na kurekebisha zichukuliwe,” akasema Bw Waita kupitia ujumbe.

Hatua hiyo ilikuja takriban saa tatu baada ya akaunti hizo kutuma ujumbe uliowaonya watu fisadi kuwa hata iwe nani, Rais hatajali ila hatamsaza.

“Ikiwa wewe ni fisadi, unaweza kuwa kaka ama dada yangu ama mwandani wangu wa karibu sana kisiasa lakini ikiwa wewe ni fisadi tutapigana nawe. Sitazuiwa na ukabila ama hadhi katika azma yangu ya kuunganisha taifa na nitaendelea kuunganisha Kenya,” ujumbe kwenye akaunti hizo ulikuwa umesema.

Baada ya kuzimwa, haingewezekana kwa yeyote kuona chochote kwenye akaunti hizo, ila mtu anapojaribu kuzitafuta hazionekani.