Njaa: Kero za wafuatiliaji habari mitandaoni
Na PETER MBURU
WAKENYA wana ghadhabu.
Hii ni baada ya vuta nikuvute kati yao na viongozi wa serikali kuhusu baa la njaa linaloendelea kuumiza wakazi wa maeneo ya Turkana, Baringo na mengine yanayokumbwa na kiangazi nchini.
Ijapokuwa serikali, ikiongozwa na Naibu Rais William Ruto na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa wamepinga kuwa kuna njaa na kuwa imeua watu, wakitaja hizo kuwa habari feki, shirika la Msalaba Mwekundu limetoa nambari ya paybill, likiwataka Wakenya kuchanga pesa kusaidia wakazi wa maeneo hayo.
Lakini kwa ghadhabu, Wakenya wamekataa kuchanga hata shilingi moja, wakisema tayari wamelipa ushuru ambao serikali inafaa kuutumia kuwalisha watu wanaoumia.
Wakenya aidha wanauliza maswali shirika hilo, wakitaka kujua ni watu gani ambao linalenga kuwasaidia, wakati serikali imezidi kushikilia kuwa ina chakula cha kutosha kwenye maghala yake na kuwa hakuna hali ya hatari.
Wakenya aidha wanataka kujua jinsi pesa ambazo shirika la Msalaba Mwekundu limekuwa likichangisha imekuwa ikizitumia, wakisema halina uwazi.
Ijumaa, waliendesha kampeni kwenye mitandao ya kijamii kwa jina #RedCrossTumechoka, kuashiria hawako tayari kuchanga pesa zozote.
“Kama mzalendo nimehakikishiwa kuwa kuna chakula cha kutosha katika ghala la kitaifa na kuwa hakuna maisha yamepotezwa ama yatapotezwa kutokana na njaa. #RedCrossTumechoka,” akasema Fredrick Musonye kwenye Twitter.
Julius Mmasi alisema “Serikali ikiongozwa na Naibu Rais Ruto, Eugene Wamalwa, Mwangi Kiunjuri na Oduor imeambia Wakenya hakuna sababu ya kuwa na taharuki, kuwa hakuna upungufu wa chakula, hakuna njaa, hakuna kifo. Red Cross watwambie huu mchango ni wa kazi gani.”
Wakenya walisema serikali imekuwa na tabia ya kuiba pesa za umma, kisha kuwarai Wakenya kuchangia mashirika fulani kutoa huduma ambazo tayari wamelipa ushuru ili wapate.
“Tumechoshwa na hii michango, tunapambana na ukosefu wa kazi, madeni, wizi na ufisadi. Hatuna nafasi ya kujali yeyote tena, kila mtu apambane na hali yake,” akasema mtumizi mmoja wa Twitter.
Baadhi ya Wakenya vilevile walishangaa jinsi serikali inalalamika kuwa changamoto kwa sasa ni usafirishaji tu, wakati imekuwa ikisafirisha vifaa vya upigaji kura na mafuta kutoka na kuelekea maeneo hayo bila tatizo.