Habari Mseto

Duale azungumzia suala la urais mwaka 2022

March 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale ameonekana kukaidi amri ya Rais Uhuru Kenyatta kwa kuendeleza siasa za urithi wa urais na uchaguzi mkuu wa 2022.

Akiongea Jumamosi mjini Mandera, Duale amewataka wakazi wa eneo hilo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya kuunga azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia Ikulu.

“Ningataka kuwahakikishia kuwa mipango ya urithi wa uongozi katika Jubilee haijabadilika. Kwa hivyo, ningependa kuwarai kumuunga mkono Dkt Ruto ifikapo mwaka 2022 ili aweze kuendeleza maendelea ambayo Jubilee ilianzisha karibia miongo miwili sasa,” akasema Mbunge huyo wa Garissa Mjini.

Kauli yake iliungwa mkono na Gavana wa Garissa Ali Roba aliyesema wakazi wa kaunti hiyo na eneo pana la Kaskazini Mashariki mwaka Kenya wako nyuma ya Dkt Ruto.

“Wakati ukitimu, tutapigia kura kwa wingi kama ambavyo tuliwapigia kura pamoja na Rais na mkashinda katika mihula miwili,” akasema gavana huyo anayehudumu kipindi chake cha pili na cha mwisho.

Mchango

Walikuwa wakiongea katika mkutano wa kuchangisha fedha za kuisaidia shule ya Madrassa mjini Mandera, shughuli ambayo iliongozwa na Dkt Ruto.

Bw Duale pia amewataka Rais Kenyatta na Dkt Ruto kutowaruhusu watu fulani wenye nia mbaya kuharibu chama cha Jubilee, ili kiweze kuongoza kwa kipindi kirefu.

Alifananisha Jubilee na chama tawala nchini Afrika Kusini, African National Congress (ANC) ambacho kimeendelea kuongoza nchi hiyo tangu taifa hilo lilipojikomboa kutoka utawala wa ubaguzi wa rangi mnamo 1994.

“Rais na naibu wake walituita mnamo 2015 na kutushauri tuvunje vyama vidogo vya kikabila ili tuunde chama kimoja chenye sura ya kitaifa. Ndipo tukaunda Jubilee ambacho wakazi wa hapa walipigia kura kwa wingi,” akasema.

Njama

Hata hivyo Bw Duale amesikitika kuwa watu wengine kutoka nje sasa wanapanga njama ya kusambaratisha chama hicho.

“Walivunja Kanu na kupelekea Rais Kenyatta kushindwa katika kinyang’anyiro cha urais mnamo 2002, kisha wakaifuatilia na Narc kisha wakabuni Cord ambayo ilivunjika kutokana na siasa mbaya. Tunawajua,” akasema.

Duale alidai kuwa uhusiano wa Rais Kenyatta na Bw Raila Odinga utaigharimu Jubilee pakubwa.

“Kama eneo, na kama mtu binafsi, tumewekeza katika chama hiki ambacho ni kama kampuni. Tumeona faida yake na bakshishi. Kama kiongozi wengine sitatizama huku Jubilee ikiharibiwa,” akasema.

Bw Duale akaongeza: “Hatutaruhusu kiongozi wa chama chetu na naibu wake kutuchezea shere kwa kutushauri kuvunja vyama vyetu kisa walete mtu mwingi kusambaratisha Jubilee,”

Kwa upande wake Dkt Ruto amewataka viongozi kujihusisha na vyama vya kisiasa ambavyo vina sura ya kitaifa na mpango wa maendeleo kwa Wakenya.

Ametaka wale “ambao wanashindana nasi” kujiondoa kutoka vyama vya kisiasa ikiwa kweli wanalenga kuliunganisha taifa.

“Hii namna ambavyo tutaeleta maendeleo nchini Kenya. Hauwezi kutoambia kwamba unaunga mkono umoja wa nchi ilhali unaongoza chama cha kikabila,” Dkt Ruto akaongeza.

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, Seneta wa Mandera Mahamud Maalim, mbunge mwakilishi wa wanawake Mandera Amina Gebow na mwenzake wa Isiolo Rehema Jaldesa.

Wengine walikuwa ni wabunge; Meja Bashir Abdullahi (Mandera Kaskazini), Ibrahim Abdi Mude (Lafey), Mohamed Dahir (Daadab), Abdikadirr Osman( Fafi), Adan Haji (Mandera Kusini) na Omar Maalim (Mandera Mashariki).