MakalaSiasa

JAMVI: Juhudi za Kalonzo kumzima Ruto Mlimani

March 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

 Na BENSON MATHEKA

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, ameanza mikakati ya kupenya eneo la Mlima Kenya, ngome ya kisiasa ya Rais Uhuru Kenyatta kama njia moja ya kuimarisha azima yake ya urais kwenye uchaguzi wa 2022.

Wadadisi wanasema ziara za Bw Musyoka ambazo zimeongezeka eneo hilo, zina baraka za wandani wa karibu na wanamikakati wa Rais Kenyatta ambao wamekuwa wakipinga azma ya Naibu Rais William Ruto.

Bw Musyoka amezuru eneo hilo mara sita katika kipindi cha mwezi mmoja na nusu akikutana na viongozi na umma katika kile ambacho wadadisi wanasema ni mikakati ya kutafuta uungwaji mkono wa azima yake ya urais.

Ziara hizo zinajiri wakati ambao, tofauti na Bw Ruto, Bw Musyoka amekuwa akiunga muafaka wa Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na vita dhidi ya ufisadi.

Bw Ruto amekuwa akitembelea eneo hilo na ameungwa mkono na wabunge kadhaa ambao wamekuwa wakiandamana naye kwenye mikutano ya harambee na ya kuzindua miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa eneo hilo katika chama cha Jubilee wamepinga vikali azima yake wakisema amekuwa akimhujumu Rais Kenyatta hasa katika vita dhidi ya ufisadi.

“Ziara za Bw Musyoka eneo la Mlima Kenya zimepangwa. Hawezi akajialika. Lengo kuu ni kumzima Bw Ruto ambaye kwa mwaka mmoja uliopita amekuwa akizuru eneo hilo kujipigia debe,” asema mdadisi wa kisiasa Nelson Kabugi.

Anasema ikizingatiwa kwamba Bw Musyoka ameunga muafaka na kwamba Bw Ruto amekuwa akiukosoa pamoja na vita dhidi ya ufisadi, wanamikakati wa Jubilee hawakuwa na jingine ila kutafuta mtu ambaye anaweza kuzima wimbi ambalo alikuwa akivumisha eneo hilo.

“Maoni yangu ni kwamba ni vigumu kuwatenga wanamikakati wa kisiasa wa Mlima Kenya na kuongezeka kwa ziara za Bw Musyoka eneo hilo. Hii ni kwa sababu zimejiri wakati ambao Bw Ruto ameanza kukosoa muafaka na vita dhidi ya ufisadi,” asema.

Katika hafla moja Kaunti ya Murang’a, Bw Musyoka alimkabili Bw Ruto kwa kukosoa vita dhidi ya ufisadi na kujitolea kumpatanisha na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Wadadisi wanasema katika ziara zake kaunti za Mlima Kenya, Bw Musyoka analenga kufufua uhusiano wake na viongozi wa eneo hilo na kuwashawishi kumuunga mkono kumrithi mwana wao Rais Kenyatta.

Huku chama cha Jubilee kikikumbwa na msukosuko wa ndani, Bw Musyoka anataka kujisawiri kama kiongozi anayeaminika kulinda maslahi ya eneo hilo akiwa rais.

“Ni kwa kuhakikishia viongozi na wakazi wa eneo la Mlima Kenya kwamba utalinda maslahi yao ukiwa rais ambapo wanaweza kukuunga mkono,” aeleza Bw Kabugi.

Kwenye ziara zake ambazo zimempeleka kaunti za Kiambu, Murang’a na Nyeri, kiongozi huyo wa Wiper amekuwa akiwakumbusha wakazi alivyomuokoa Rais Mwai Kibaki kwa kushirikiana naye kuunda serikali baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata 2007.

Wandani wa Bw Musyoka wanasema kwamba ziara zake eneo hilo zinalenga kushawishi wakazi kumuunga mkono baada ya mwana wao Rais Kenyatta kukamilisha kipindi chake cha pili.

Kulingana na mbunge wa Mwingi Magharibi, Charles Nguna, Bw Musyoka anataka kurithi ngome ya kisiasa ya Rais Kenyatta. Viongozi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakimpiga vita Bw Ruto mwaka huu walihudhuria hafla mbili za kisiasa za Bw Musyoka Ukambani na kuashiria kuwa wako tayari kushirikiana naye kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Hii ni baada ya kuibuka kuwa huenda Rais Kenyatta hatamuunga mkono Bw Ruto kugombea urais 2022. Mmoja wa waliohudhuria kongamano la viongozi wa Wiper nyumbani kwa Bw Musyoka mapema mwaka huu ni aliyekuwa naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe ambaye anatoka Murang’a. Bw Murathe ameapa kumzuia Bw Ruto kugombea urais.

Kulingana na Bw Nguna, jamii ya Wakamba na ya Wakikuyu ni majirani na Bw Musyoka anaamini kwamba zinafaa kushirikiana.

“Tunachofanya (kama wiper) ni kuzungumza na ndugu zetu kutoka eneo la Kati la Kenya na kuwakumbusha kuwa sisi si majirani pekee bali ni marafiki ambao ushirikiano kama jamii ulianza miongo mingi iliyopita,” alisema Bw Nguna.

Kulingana na mbunge wa Gatanga Nduati Ngugi ambaye alimwalika Bw Musyoka katika wadi ya Kariara mwezi jana alisema makamu huyo wa zamani wa rais amekuwa mstari wa mbele kuhimiza Wakenya kuishi kwa amani.

Wadadisi wanasema kwamba Wakenya watasubiri kuona iwapo juhudi za Bw Musyoka zitazaa matunda. Anatarajiwa kutembelea kaunti za Meru na Tharaka Nithi katika juhudi za kushawishi jamii za Gema kumuunga mkono.