Makala

TAHARIRI: Mabilioni ya kazi gani kama watu wafa njaa?

March 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

Habari zilizoshamiri wiki hii inayokamilika ni suala la njaa na haswa ripoti za vifo vilivyotokana na baa la njaa linaloshuhudiwa katika kaunti 12 zikijumuisha Baringo, Turkana na Samburu.

Baada ya picha za awali kusambazwa mitandaoni zikionyesha hali ya kutamausha katika eneo la Tiaty, Kaunti ya Baringo, serikali kupitia Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa ilijitokeza na kukanusha ripoti kwamba wakazi wa eneo hilo wanakufa na njaa.

Badala yake, na katika hatua iliyosisitizwa na Naibu Rais William Ruto baadaye Jumatano, ni kwamba kuna kiangazi cha muda mrefu na kwamba chakula kipo, tatizo pekee likiwa kukifikisha katika maeneo yanayokihitaji.

Ni jambo lililozua mjadala mkali, haswa ikizingatiwa kwamba vikosi mbali mbali vya wanahabari vilikuwa vimefika kwenye maeneo yenyewe yaliyoripotiwa kukumbwa na maafa kwa sababu ya njaa, na wakajionea wenyewe hali ilivyokuwa.

Kufikia sasa, hata hivyo, hakuna ubishi kwamba maeneo kadhaa nchini yanakumbwa na baa la njaa. Na hapa ndipo darubini inamulika serikali ya kitaifa na ile zile za kaunti. Habari za baa la njaa kamwe sio habari chipuka, la.

Baa la njaa huibuka kutokana na msururu wa matukio unaoanza na mvua kuwa haba, mimea kutofanya vizuri kwa sababu ya kiangazi au maradhi, mito kukauka na kufanya chakula cha binadamu na mifugo kuwa haba hadi mpaka pale jamii zinaanza kupungukiwa na chakula majumbani mwao.

Ni matukio yanayochukua miezi. Hivyo basi, kwa viongozi kubumburuka sasa hivi kana kwamba ni tukio lililochipuka usiku wa manane ni kejeli kubwa na dhihaka kwa umma.

Zaidi ni kukumbuka kwamba serikali zimegatuliwa kwa ajili ya kumfikia mwananchi kwa urahisi. Zinafanya nini hizi serikali ambazo hazijui wananchi wake wanakodolea kifo kutokana na baa la njaa?

Mabilioni yanayogawanywa kila mwaka wa kifedha yanafanya kazi gani kama hayawezi kutatua mahitaji ya kimsingi kama kulisha umma wake?

Hivi, viongozi wana utu kweli, kufanya ziara kwenye ndege zao za helikopta na kujivinjari kwenye mikahawa ya kifahari mijini ilhali wakazi katika maeneo yao mara ya mwisho walipoona chakula ilikuwa wiki iliyopita?

Ni wazi kwamba taifa la Kenya limepitia majanga mengi kuanzia machafuko ya kisiasa, na wizi wa fedha za mlipa ushuru kila uchao kiasi kwamba kuna hisia za kukata tamaa miongoni mwa wengi. Kile hata hivyo hatupaswi kuchoka kuzungumzia ni jukumu la serikali kushughulikia mahitaji ya kimsingi.