• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Msaada kwa wanawake wa gereza la Thika

Msaada kwa wanawake wa gereza la Thika

Na LAWRENCE ONGARO

WANAWAKE walio na watoto wachanga gerezani nchini wamekuwa wakikosa msaada wa dharura kutokana na mazingira ya jela.

Lakini Bi Shekinah Mutilili, wa miaka 15 wa shule ya Upili ya BrookHouse School kwa ushirikiano na wanafunzi wa shule hiyo pamoja na wahisani wengine wamejitolea kuwapa misaada wanawake wafungwa walio na watoto wadogo.

Mnamo Jumamosi walizuru gereza la Thika na kuwafadhili wanawake walio magerezani na vifaa muhimu vya kuwafaa na watoto wao.

Anasema wamejitolea kwa mwito unaotajwa kama ‘Freedom With Hinke’ huku lengo kuu ni kuinua hadhi ya mtu katika Umma.

Wakati wa kuzuru gereza hiyo ya Thika, waliweza kutoa misaada ya vifaa muhimu vya watoto vya Pampers, sabuni, mafuta ya kujipaka na vipodozi vingine.

Walitoa vikombe, sodo na vipodozi muhimu kwa wanawake.

“Hiyo ilikuwa ndoto yangu kwani kwa muda mrefu nimekuwa nikiwahurumia wanawake walio na watoto wachanga gerezani,” alisema Binti Mutilili.

Bi Elizabeth Irungu wa miaka 28 aliyefungwa miaka 4 katika gereza hiyo kwa mauaji ana mtoto mdogo wa miaka miwili.

Anasema maisha ya gereza sio rahisi ukiwa na mtoto mchanga. “Hapa mambo sio rahisi kwani huwezi kupata mahitaji yote unayohitaji kwa hivyo ni kuvumilia tu,” alisema Bi Irungu.

Naye Maureen Murugi, wa miaka 27 kutoka Embu, ni mfungwa anayetumikia kifungo cha miaka miwili kutokana na wizi wa pesa huku akidai alisingiziwa bure.

“Mimi niko na mtoto mchanga wa mwaka moja ambaye nilijifungua miezi minne tu baada ya kufungwa jela. Mtoto wangu kwa sasa anakosa mahitaji muhimu kama lishe bora lakini mambo ni kuvumilia hadi mwisho,” alisema Bi Murugi.

Naye Mary Waceke Muya, ambaye pia ni mmoja wa wafadhili wa misaada hiyo anasema mtoto mdogo hafai kupata shida pamoja na mamake akiwa gerezani.

“Ni vyema watoto kujengewa kituo cha chekechea ambacho kitawapa mwongozo wa kimasomo wakiwa gerezani,” alisema Bi Muya.

Alisema mtoto mdogo anastahili kupata mazingira mema ya nje ili akili yake ikue inavyostahili. “Iwapo mtoto mdogo hapati kucheza na watoto wenzake bila shaka hata akili yake haiwezi fikiria ipasavyo,” alisema Bi Muya.

Afisa mkuu wa magereza ya wanawake Bi MaryAnne Mutembei, alishukuru kuletewa misaada hiyo katika gereza lake hapa Thika akisema ni hatua ya heshima.

“Hata kituo cha chekechea tayari kimejegwa kwa uwezo wa wafadhili hawa huku pia wakitoa tangi kubwa la maji linalohifadhi lita 10,000 kwa wakati moja,” alisema Bi Mutembei na kuongeza, Sisi tunawapongeza kwa dhati kwa kazi nzuri waliyofanya ambapo kama watazuru magereza mengine litakuwa jambo la busara.

You can share this post!

TAHARIRI: Mabilioni ya kazi gani kama watu wafa njaa?

Mitetemeko ya ardhi yazua hofu nchini

adminleo