Habari Mseto

MKU, Makerere waingia katika ushirikiano kielimu

March 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE  ONGARO

CHUO Kikuu cha Makerere cha Uganda na kile cha Mount Kenya (MKU) zitafanya utafiti wa pamoja kwa minajili ya  kupambana na changamoto kadha Afrika Mashariki na Kati.

Azimio hilo lilipitishwa mnamo Jumatatu mjini Thika wakati ujumbe wa wasomi kutoka Makere ulizuru MKU mjini Thika kupitisha kauli hiyo iliyokuwa imeafikiwa Januari 2019 jijini Kampala, Uganda.

Dkt Bibianne Waiganjo wa kitengo cha utafiti na masomo, alisema vyuo hivyo viwili vitazingatia utafiti kuhusu saratani na kisukari; maradhi ambayo yamekuwa tishio kubwa kwa maisha ya binadamu.

Alisema muungano huo wa utafiti pia utaangazia masomo ya uhifadhi wa chakula, maswala ya ubunifu na biashara.

Alisema ushirikiano huo wa vyuo viwili utahakikisha vimeibuka na ubunifu wa kutegemewa kuhusu maswala ya saratani katika utafiti wao.

“Tutahakikisha  ushirikiano huo una toka na jambo la  kuaminika   ili kuona ya kwamba janga hilo la  saratani  linapunguzwa kutokana na kuangamiza  idadi kubwa ya  watu,” alisema Dkt Waiganjo.

Alisema kando na utafiti huo bado watajizatiti kuona ya kwamba vyuo hivyo vinafanya juhudi kuchunguza magonjwa mengine ambayo ni hatari kwa  binadamu.

Aidha, alisema kuna haja pia kuona ya kwamba masomo katika vyuo hivyo viwili yanaboreshwa kwa kiwango kikubwa huku wanafunzi wa pande zote mbili wakifanya mipango ya kubadilishana mawazo kwa kutembeleana vyuoni mwao.

Alisema kwa sababu Makerere ni chuo kilichoanzishwa kitambo, kina wingi wa ujuzi kimasomo na kwa hivyo Chuo cha Mount Kenya kinaweza kikapata ujuzi zaidi kutoka huko.

Mwongozo

Mkurugenzi wa maswala ya utafifi katika Chuo cha Makerere Profesa Muhadasi Buyiza, alisema vyuo vyote viwili vinastahili kuketi chini pamoja na kuja na mwongozo wa kuaminika katika utafiti wao ambao umeangaziwa sana.

Naye mkuu wa kitengo cha afya katika Chuo Kikuu cha Makerere Profesa Charles Ibingira alitaka vyuo hivyo kuja pamoja na kutoka  na jambo muhimu litakalokuwa na umuhimu wake kwa wanafunzi wengine.

Profesa Francis Muregi, mkurugenzi wa utafiti MKU alisema baada ya makubaliano, matokeo ya utafiti yatachunguzwa  kutoka kila eneo ili kuzifanyia uwiyano.

Wengine waliozuru Kenya kutoka Uganda ni Prof Fred Masagazi, Mkuu wa elimu na masomo ya nje, na Prof Tonny Oyana ambaye ni mkuu wa mitandao na masomo ya nje.

Wengine ni Prof Peter Wanderi wa MKU, na mkurugenzi wa maswala ya masoko Bw Boniface Murigi.